Naibu Waziri Aweso Atoa Onyo Kali Kwa Mkandarasi Muleba

Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso ametoa onyo kali kwa Mkandarasi anayefanya kazi ya ujenzi wa Mradi wa Maji Katoke, Wilaya ya Muleba DC, mkoani Kagera baada kubaini changamoto mbalimbali katika mradi huo.

Mradi huo ambao umegharimu kiasi cha zaidi ya Shilingi milioni 476, umeonekana kuwa na kasoro mbalimbali licha ya kukamilika kwake, jambo lililomfanya Naibu Waziri kukasirishwa na Mkandarasi.

Naibu Waziri Aweso amemtaka Mkandarasi huyo awepo kwenye eneo la mradi, atakapofika kuukagua mradi huo, ambaye licha ya kuandikiwa barua tano zikimtaka kufanya marekebisho, bado amekuwa hafiki eneo la mradi na kufanya marekebisho stahiki.

Amesema ni lazima mkandarasi huyo afike na kueleza ni kwanini mradi huo una matatizo, pamoja na kuwa umekamilika unakosa thamani halisi ya fedha (value for money) zilizotumika kujenga mradi huo.

Ikibainika kuna ubadhirifu wa fedha hatua kali zitachukuliwa ikiwemo kuwafukuza wote kazi Mkandarasi na Mhandisi wa Wilaya, pamoja na kuwafikisha katika vyombo vya sheria kwa ajili ya kuchukuliwa hatua.

“Niwaonye watendaji wa Sekta ya Maji, hakikisheni mnawapa kazi wakandarasi wenye uwezo ambao watafanya kazi nzuri na kisha kuidai Serikali malipo yao; sio wakandarasi wajanja ambao wamekuwa wakila fedha za Serikali kiholela bila matokeo kuonekana”, alionya Aweso.

“Ndio maana nimefika Kagera kujionea fedha ambazo wizara inazitoa kama zinaleta matokeo na sio kuchezewa, huku kilio cha wananchi cha huduma ya majisafi na salama kikiendelea. Jambo hilo halina nafasi  kwenye Serikali ya Awamu ya Tano na Wizara ya Maji kwa sasa”, alisisitiza Aweso.

Akatoa tahadhari kwa kusema kuwa tunapoelekea kuanzisha Wakala wa Maji Vijijini (RUWA) wahandisi wababaishaji hawatakuwa na nafasi. Wizara itahakikisha inafanya utaratibu wa kuhakiki uwezo wa wahandisi wote wa maji na kuondoa wazembe na wanaokosa uadilifu.

Naibu Waziri Aweso atakua ziarani Kagera kwa siku tano kukagua miradi ya maji na kutatua changamoto.


from MPEKUZI

Comments