Mzee wa Miaka 80 Auawa na Kunyofolewa Sehemu zake za Siri

Watu wawili wamefariki  dunia mkoani Kagera katika matukio mawili tofauti, likiwamo la mzee mmoja aliyejulikana kwa jina la Laurian Kakoto (80), mkazi wa kijiji cha Ihunga kata Kishanda wilayani Muleba, kukatwa sehemu zake za siri na wahusika kuondoka nazo.

Akizungumza na waandishi wa habari, kamanda wa polisi mkoani Kagera Revocatus Malimi amesema kuwa baba huyo aliondoka nyumbani Januari 7 mwaka huu kwenda kuhemea lakini hakurudi hadi maiti yake ilipogunduliwa na wananchi ikiwa imezikwa huku nyayo za miguu zikiwa zinaonekana juu ya kaburi, Januari 08 saa moja asubuhi.

Kamanda Malimi amesema kuwa baada ya wananchi kugundua tukio hilo walitoa taarifa polisi, ambapo walifika na kufukua mwili huo uliokuwa umezikwa kwa kutanguliza kichwa chini, na kukuta amekatwa kwa kitu chenye ncha kali shingoni na sehemu za siri.

Aidha kamanda huyo amesema kuwa jeshi la polisi linaendelea kuwasaka wananchi waliojichukuliwa sheria mkononi kwa kuchoma moto nyumba 16 na kufyeka migomba, mali za watu waliowatuhumu kumuua mwendesha bodaboda mmoja Albert Antipas, aliyetoweka tangu Januari 02 mwaka huu na maiti yake kupatikana ikiwa katika bwawa la kufugia samaki, Januari 07.

Amesema kuwa maiti ya mwendesha bodaboda huyo ilikutwa ikiwa imefungwa kwa kamba mikononi na miguuni, na kisha kufungwa katika jiwe na kuzamishwa katika bwawa hilo. 

Baada ya wananchi wa kijiji cha Kibingo tarafa ya Murongo wilayani Kyerwa kusikia kuwa watuhumiwa wamekamatwa na polisi, ndipo walipokwenda kuchoma moto nyumba zao.


from MPEKUZI

Comments