Mawakala ATCL Kuendelea Kusota Rumande

Upande wa utetezi katika kesi ya mawakala wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), wanaokabiliwa na mashtaka ya utakatishaji fedha na kulisababishia shirika hilo hasara ya Sh. milioni 10.8, umelalamika ucheleweshaji wa upelelezi na kusababisha washtakiwa kukaa mahabusu kwa muda mrefu.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni Farian Ishengoma (34), ambaye ni mtaalamu wa hali ya hewa, mawakala wa ndege, Neema Kisunda (24), Alexander Malongo (29), Tunu Kiluvya (32) na Job Mkumbwa (30).

Wengine ni wafanyabiashara Adam Kamara (27), Marlon Masubo (29), Mohammed Issah (38), mkazi wa Yoruba Nigeria, Godfrey Mgomela, Absalom Njusi na Janeth Lubega, ambao walifikishwa mahakamani hapo jana na kusomewa mashtaka yao mbele ya Hakimu Mkazi, Salum Ally.

Shauri lao lilifikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi, Janeth Mtega.

Wakili wa Serikali, Ester Martin, alidai kuwa, kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kutajwa na upelelezi bado unaendelea na kuiomba mahakama kupanga tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa kwa shauri hilo.

Wakili wa utetezi, Augustine Kulwa, aliuomba upande wa serikali kuharakisha upelelezi kwa madai kuwa washtakiwa hao wamekaa muda mrefu mahabusu.

Hakimu Mtega aliahirisha kesi hiyo hadi Januari 17, mwaka huu, itakapotajwa tena.

Washtakiwa hao wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Machi 10 na Oktoba 9, mwaka jana, katika maeneo ya Dar es Salaam na Mwanza kwa pamoja wakiwa mawakala wa ATCL na kulisababishia shirika hilo hasara ya Sh. 10,874,280.

Katika mashtaka ya pili, inadaiwa kati ya Machi 10 na Oktoba 9, mwaka jana katika maeneo ya Dar es Salaam na Mwanza kwa udanganyifu walijipatia fedha hizo kutoka kwa wateja mbalimbali wa ATCL kwa kuwadanganya kuwa watawakatia tiketi.

Pia alidai kati ya tarehe hizo na maeneo hayo, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kuwa walijipatia Sh.10,874,280 mali ya ATCL wakati wakijua kuwa fedha hizo ni zao la uhalifu.

Washtakiwa hao hawakutakiwa kujibu chochote kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kisheria kusikiliza kesi hiyo hadi upelelezi utakapokamilika na kwenda kusikilizwa Mahakama Kuu.

Washtakiwa wamerudishwa rumande hadi Januari 17, mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa tena.



from MPEKUZI

Comments