Mahakama Yawafutia Kesi aliyekuwa Kamishina Mkuu wa Mamlaka ya Mapato (TRA), Harry Kitillya na wenzake

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewafutia mashtaka aliyekuwa Kamishina Mkuu wa Mamlaka ya Mapato (TRA), Harry Kitillya na mwenzake wawili ambao ni maofisa wa benki ya Stanbic, Shose Sinare na Sioi Solomon.

Washtakiwa hao walikuwa wanakabiliwa na mashtaka nane yakiwemo ya kutakatisha fedha.

Wamefutiwa kesi hiyo chini ya kifungu namba 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya jinai (CPA), sura ya 20, iliyofanyiwa marejeo mwaka 2002.

Uamuzi huo imefikiwa leo Januari 11 na Hakimu Mkazi, Salum Ally baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kueleza mahakama hiyo kuwa hana nia ya kuendelea na shauri hilo.

Wakili Mkuu wa Serikali, Hashimu Ngole akisaidia na wenzake Pendo Mangole na Patrick Mwida, amedai mahakamani hapo kuwa DPP hana nia ya kuendelea na shauri hilo dhidi ya washtakiwa hao.

"Taarifa hii ya kutokuendelea na shauri hili mbele ya mahakama yako, imeletwa chini kifungu namba 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), sura ya 20, iliyofanyiwa marejeo mwaka 2002," amesema Ngole.

Baada ya maelezo hayo, Hakimu Ally alisema kutokana na maombi hayo, mahakama hiyo imeifuta kesi hiyo.

Hata hivyo, washtakiwa hao baada ya kufutiwa kesi hiyo, wamekamatwa tena na kuwekwa mahabusu.


from MPEKUZI

Comments