Lugola: Serikali Itawashughulikia Viongozi Wa Dini Waliojipenyeza Kuanzisha Makanisa Na Misikiti Kwa Lengo La Kufanya Uchochezi

Na Felix Mwagara, MOHA-Ngara.
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amesema baadhi ya viongozi wa dini nchini wamejipenyeza na kuanzisha makanisa na misikiti kwa lengo la kuanzisha vichaka vya kujificha ili tujue ni watu wa Mungu kumbe wanataka kufanya uchochezi na kuvuruga amani nchini. 
 
Lugola amesema Serikali ya Rais Dkt. John Magufuli haitawavumilia wale wote walioanzisha taasisi hizo kwa lengo lao binafsi na itahakikisha inawashughulikia ipasavyo bila kuwaonea huruma.
 
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliohudhuriwa na mamia ya wananchi wa Mji wa Ngara, jana, Lugola alisema makanisa na misikiti ambayo imesajiliwa na Wizara yake hatakubali kuona viongozi hao ambao wanajifanya kuwa na watu wa Mungu kumbe wanamalengo hayo binafsi.
 
“Makanisa na miskiti itakayobainika ina malengo hayo, sitaona haya kuifutia usajili, na pia nawataka viongozi wa dini endapo migogoro inaibuka hakikisheni  mnaitatua wenyewe kwa amani,” alisema Lugola.
 
Lugola aliongeza kuwa, Serikali inaheshimu imani ya dini na pia viongozi wao wanamchango mkubwa katika maendeleo ya nchi kutokakana na maombi pamoja na kuwaongoza waumini wao vizuri, lakini pia wapo baadhi ya viongozi hao wa dini, wanaingiza masuala ya siasa makanisani na misikitini.
 
“Niwaombe na niwatake viongozi wote wa dini, wakati tunapoenda katika uchaguzi, viongozi wa makanisa na misikiti iliyosajiliwa, niwaombe pale migogoro inapoibuka hakikisheni mnaitatua wenyewe kwa amani na msiruhusu mtu ambaye ana nia mbaya na maendeleo ya nchi hii, aje kuwaingilia,” alisema Lugola. 
 
Aidha, Waziri Lugola katika mkutano huo aliitaka Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) apitie upya usajili na utoaji wa vitambulisho vya taifa katika mikoa ya Kagera na Kigoma ili waweze kuwabaini  na kuwaondoa raia wa nchi jirani zinazoizunguka mikoa hiyo.
 
Pia Lugola, alimpa wiki mbili  Kamishna Jenerali wa Uhamiaji nchini, awe amefika katika mikoa hiyo kwa ajili ya kuanza maandalizi ya kufanya operesheni kubwa ya kuwaondoa Wahamiaji haramu katika Mikoa hiyo kabla ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kuanza mwezi Julai mwaka huu.
 
Lugola aliongeza kuwa, licha ya kutangaza operesheni hiyo, lakini viongozi wa uhamiaji katika mikoa hiyo wawe makini mara kwa mara kuhakikisha wanawafuatilia wahamiaji hao kwa kuwashirikisha wananchi waaminifu ili waweze kutoa taarfia sahihi za wahamiaji hao.


from MPEKUZI

Comments