KCMC Yasitisha Kutoa Huduma ya Bima Kwa Makampuni Haya

Hospitali  ya Rufaa ya KCMC iliyopo mkoani Kilimanjaro imesitisha kutoa huduma kwa wafanyakazi wa makampuni saba yanayotumia bima za afya kutokana makapuni hayo kudaiwa zaidi ya shilingi bilioni 2.2.
 
Kwa mujibu wa Ofisa Habari na Mahusiano wa KCMC, Gabriel Chisseo, hospitali hiyo imelazimika kuchukua uamuzi huo baada ya makampuni hayo kushindwa kulipa madeni yake  yanayokadiliwa kufikia Sh. Bilioni 2.2.
 
Chisseo ameyataja Makampuni hayo kuwa  ni NSSF, AAR, Jubilee, Strategies, Ngorongoro, TPC na TANESCO ambapo amesema  baadhi yake yanadaiwa fedha za tangu mwaka 2016.
 
“Tuna mkataba na hizi taasisi, ule mkataba unaonyesha baada ya mwezi mmoja wawe wametulipa baada ya kutoa huduma kwa wanufaika wao, hadi sasa tuna madai ya tangu mwaka 2016 mpaka sasa.
 
“Kwa hiyo kwetu sisi tunapata mzigo mkubwa na wakumbuke
tumekuwa tuna jukumu la kutibu watanzania ambao hawana uwezo kupitia hiki hiki kiasi kidogo ambacho wananchi wamekuwa wanachangia,” alisema Chiseo.
 
Alisema uongozi wa hospitali umeshatoa taarifa kwa njia mbalimbali, hivyo ni wajibu wa wanufaika hao kwenda moja kwa moja katika taasisi na mashirika hayo kuwaeleza namna ambavyo wataweza kuhudumiwa baada ya huduma kusitishwa.


from MPEKUZI

Comments