Katibu Mkuu CCM Dkt. Bashiru Awataka Watumishi Wa Serikali Kujifunza Kufanya Maamuzi Kutoka Kwa Rais Magufuli

Na Stella Kalinga, Simiyu
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Dkt. Bashiru Ally amewataka Watumishi wa Serikali  kujifunza kufanya maamuzi  kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, kwa ajili ya maslahi mapana ya Taifa.

Dkt. Bashiru ameyasema hayo mjini Bariadi katika kikao na Wakurugenzi wa Taasisi zitakazoshirikiana na Mfuko wa Taifa wa  Bima ya Afya (NHIF) na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) kujenga kiwanda cha (vifaa tiba) bidhaa za afya zitokanazo na pamba wilayani Bariadi, baadhi ya viongozi, watendaji wa Chama na Serikali na  wawekezaji katika zao la pamba mkoani Simiyu, ambacho kililenga kujadili ujenzi wa kiwanda hicho na mnyororo wa thamani wa zao la pamba.

Dkt. Bashiru  amesema watumishi wa serikali waache tabia ya kuzungumza bila kutenda badala yake wawe na moyo wa uzalendo na wafanye maamuzi sahihi kwa muda muafaka huku akisisitiza kuwa hawapaswi kuwa sehemu ya vikwazo katika  maamuzi ya utekelezaji wa shughuli za miradi ya maendeleo.

“Watumishi wa Serikali jifunzeni kutoka  kwenye tabia ya Rais wetu, fanyeni maamuzi kwa maslahi mapana ya Taifa, muwe na moyo wa uzalendo na ujasiri katika kuchukua maamuzi; maamuzi hayo yafanyike kwa usahihi kwa muda muafaka” alisema Dkt.. Bashiru.

Kuhusu ujenzi wa kiwanda cha bidhaa za afya zinazotokana na zao la pamba mkoani Simiyu, Dkt. Bashiru alioneshwa kutoridhishwa na kasi ya maandalizi ya ujenzi huo  na   kumwagiza Mkurugenzi wa kituo cha uwekezaji (TIC), Bw. Godfrey Mwambe  kuratibu mazungumzo ya kuwakutanisha wahusika wote ili utekelezaji wa mradi uanze mara moja.

“Tulikubaliana kazi itaanza Desemba 2018 na Desemba imeshapita, tumedhamiria na tumeshatamka kuwa tutajenga viwanda, hatuwezi tukakwamisha mipango ya kujenga viwanda na wakati tumeamua kujenga uchumi wa viwanda hapana; Tarehe 09 Januari saa 3:00 asubuhi wale wote wanaohusika na ujenzi wa kiwanda hiki tukutane Lumumba tuzungumze” alisema Dkt. Bashiru.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amesema ni vema viongozi wa Serikali wanaohusika katika kutoa maamuzi yatakayopelekea ujenzi wa kiwanda cha bidhaa za afya zitokanazo na pamba  wachukue hatua,  ili ujenzi uanze mara moja  na wamiliki wa viwanda vya kuchambua pamba waanze kujua mahitaji ya pamba itakayotumika na kiwanda hicho katika msimu wa mwaka 2018/2019.

“Yapo mambo tulikubaliana kufikia Desemba 2018 yawe yamekamilika, tunaomba kama kuna mambo bado yako mezani yaondoke jambo hili liweze kusogea, taratibu za manunuzi zianze ili hatua za kutengeneza mashine zifanyike na kupitia pamba itakayoanza kununuliwa mwezi Mei, wamiliki wa viwanda vya kuchambua pamba waanze kujua mahitaji ya kiwanda katika msimu wa mwaka 2018/2019, ili kiwanda kisije kikakamilika pamba ikakakosekana” alisema Mtaka.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Pamba Tanzania, Bw. Marco Mtunga amesema upatikanaji wa malighafi ya kiwanda cha vifaa tiba (bidhaa za afya zitokanazo na zao la pamba)  kinachotarajiwa kujengwa Bariadi ni wa uhakika na kubainisha kuwa Bodi hiyo imejiwekea malengo ya kuzalisha tani milioni moja ifikapo mwaka 2022.

Mkurugenzi wa Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya(NHIF), Bernad Konga amesema tayari bodi ya mfuko huo imeshatenga kiasi cha shilingi bilioni kumi kwa ajili ya kuwekeza katika  ujenzi wa kiwanda cha (vifaa tiba) bidhaa za afya zitokanazo na pamba mkoani Simiyu, lengo likiwa ni kupunguza gharama za kuagiza bidhaa hizo nje ya nchi na kuongeza thamani ya zao la pamba nchini.

Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa(MSD), Bw. Laurian Rugambwa amesema bidhaa za afya zitokanazo zao la pamba zitakazozalishwa na kiwanda hicho zitapata soko la uhakika katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara(SADC) na hapa nchini kupitia Bohari hiyo, kwa kuwa sasa bidhaa hizo zinaagizwa nje ya nchi.

Baadhi ya wawekezaji wa viwanda vya kuchambua pamba mkoani Simiyu wamesema pamoja na kujenga kiwanda cha bidhaa za afya zitokanazo na pamba njia kuu ya kuongeza thamani ya zao la pamba ni kujenga viwanda vya nyuzi na nguo, huku wadau wa wakitoa maoni yao

“Tunapaswa kuongeza thamani ya zao la pamba ili wakulima waweze kunufaika na uzalishaji wanaofanya, moja ya njia kuu ya kuongeza thamani ni uwekezaji katika viwanda vya nyuzi na nguo, huu ni uwekezaji mkubwa unaotoa ajira nyingi, Serikali ingalie upya sera, sheria na kodi zinazogusa uwekezaji katika eneo hili” alisema Salum Khamis mwekezaji Shinyanga.

“Ipo haja ya kwenda kwenye uwekezaji katika viwanda vya nyuzi na nguo hapa nchini  na kwa sababu sisi ni miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa pamba Afrika, tukitegemea sana soko la nje kwa siku zijazo tunaweza kukwama hasa katika suala bei ya pamba” alisema Boaz Ogola Kiwanda cha Kuchambua pamba cha Alliance Ginnery.

Kiwanda cha Bidhaa za afya zitokanazo na zao la pamba kinatarajiwa kujengwa mwaka huu 2019 katika Kata ya Dutwa wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), ambapo ujenzi huo umeshirikisha Taasisi nyingine za Umma ambazo ni wadau muhimu katika kufanikisha utekelezaji wa mradi huo kwa ufanisi.

Taasisi hizo ni Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda (TIRDO), Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Benki ya Uwekezaji Tanzania (TIB Corporate) na Bohari ya Dawa  ya Taifa (MSD).


from MPEKUZI

Comments