Jeshi la Polisi: Matukio ya mauaji ya ulevi , Watoto Kuibiwa Yamepungua

Jeshi la Polisi limesema matukio ya mauaji yatokanayo na ulevi nchini yamepungua kutoka makosa 129 yaliyoripotiwa mwaka 2017 hadi makosa 118 mwaka jana, ambayo ni sawa na upungufu wa asilimia 8.8.

Pia, matukio ya kupotea ama kuibiwa kwa watoto yamepungua kutoka matukio 134 yaliyoripotiwa mwaka 2017 hadi makosa 116 yaliyotokea mwaka jana, ikiwa ni upungufu wa asilimia 13.4.

Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Ahmed Msangi, aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu masuala mbalimbali.

“Takwimu zinaonyesha kuwa matukio ya mauaji yanayotokana na ulevi yamepungua. Kwa kipindi cha Januari hadi Desemba matukio hayo yamepungua, ambapo kwa mwaka 2018 yalikuwa matukio 118, ukilinganisha na mwaka 2017 yaliripotiwa matukio 129, ikiwa ni upungufu wa mkosa 11 sawa na asilimia 8.8,” alisema Msangi.

Msangi alisema Jeshi la Polisi linatoa wito kwa watumiaji wa kilevi kunywa kwa kiasi na kujiepusha na matukio ya ugomvi pindi wanapokuwa wamelewa.

Kuhusu matukio ya kupotea kwa watoto, Msangi alisema mwaka 2017 kuliibuka vitendo vya kuibiwa kwa watoto ama kupotea hali iliyosababisha hofu kwa jamii hususani kwa wazazi na walezi.

“Kuhusu matukio ya kupotea au kuibiwa kwa watoto nayo yamepungua, kwa mwaka 2017 matukio yaliyoripotiwa yalikuwa 134, lakini mwaka 2018 yalipungua hadi kufikia matukio 116 ikiwa ni upungufu wa matukio 18 sawa na asilimia 13,” alisema Msangi.

Alisema licha ya kupungua kwa matukio hayo, Jeshi la Polisi linatoa tahadhari kwa wazazi kutowaacha watoto kutembea peke yao, pamoja na kuwa makini na watu wasiowafahamu kuwaachia watoto.

Kuhusu matukio ya usalama barabarani, Msangi alisema matukio hayo nayo yamepungua ambapo kwa mwaka 2017 yalitokea matukio 6,022 kulinganisha na mwaka jana, ambapo yalitokea makosa 3,988 ikiwa ni pungufu ya matukio 2,034 sawa na asilimia 33.8

“Kupungua kwa matukio hayo kumeonyesha kuwa kuna juhudi za Jeshi la Polisi kupambana na matukio hayo,” alisema Msangi.

Alisema Jeshi la Polisi linatoa wito kwa taasisi mbalimbali zikiwamo za serikali, vyama vya siasa, asasi za kiraia, asasi za kidini na Watanzania wote kuendelea kutoa taarifa za kukabiliana na matukio ya uhalifu nchini.



from MPEKUZI

Comments