TTCL yasaini na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote kupeleka huduma vijijini Katika Kara 173

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe ameshuhudia hafla ya utiaji saini baina ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) na kampuni nne za simu za mkononi ambazo zimepatiwa ruzuku na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya shilingi bilioni 173 ya kupeleka huduma za mawasiliano vijijini kwenye kata 173  zilizopo kwenye maeneo mbali mbali nchi nzima.

 Kampuni nne zilizosaini mkataba na UCSAF ya kupeleka mawasiliano ni Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Kampuni ya Vodacom Tanzania, Kampuni ya Viettel Tanzania (Halotel) na Kampuni ya MIC Tanzania (TIGO).

Wakati akishuhudia utiaji saini huo, Mhandisi Kamwelwe amesema kuwa dunia hivi sasa iko kiganjani ambapo kila mwananchi anatakiwa apate mawasiliano ya uhakika kama ambavyo Ilani ya Chama cha Mapinduzi inavyotutaka tuhakikishe tunawapatia watanzania wote huduma za mawasiliano

“Tumekubaliana na Shirika la Posta Tanzania (TPC) kuwa waanze kutoa huduma za kifedha na watumie huduma za Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) ili mawasiliano yaweze kufika vijijini kwa kuwa TPC na TTCL ni taasisi kongwe na wana mtandao mpana wa ofisi zao nchi nzima”, amesema Kamwelwe.

Ameongeza kuwa kampuni za simu za mkononi zililenga zaidi kutoa huduma za mawasiliano mijini ila Serikali ikaone ni muhimu ianzishe Mfuko wa UCSAF ili ipeleke mawasiliano kwa wananchi wote vijijini na kwenye maeneo ambayo hayana mvuto wa kibiashara 

“Sasa tuna TTCL, lengo ni kuhakikisha  kuwa TTCL inaenda kila kona kwa kuwa hizi fedha za ruzuku tunazowapa kampuni za simu za mkononi ni za walipa kodi,” amefafanua Kamwelwe. Amesema kuwa tunataka wajenge minara ya simu za mkononi kwenye maeneo yaliyoainishwa kwa kuwa yale ni maeneo ya ndani kabisa  ili kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2020 kusiwe na mwananchi ambaye hapati mawasiliano

Naye Mtendaji Mkuu wa UCSAF Mhandisi Peter Ulanga amesema kuwa kampuni nne za mawasiliano za simu za mkononi zimeshinda zabuni ya Awamu ya Tatu ya kupeleka mawasiliano kwenye kata 178 kwa gharama ya shilingi bilioni 28. Mhandisi Ulanga ameongeza kuwa hadi hivi sasa UCSAF imepeleka mawasiliano kwenye jumla ya kata 703 nchi nzima kwa kujumuisha awamu za awali za mradi

Amefafanua kuwa UCSAF imefikisha huduma za mawasiliano kwa wananchi walio wengi ambao awali hawakuwahi kuwa na huduma hiyo muhimu ambapo imeboresha maisha ya wananchi kupitia TEHAMA

Akizungumza bada ya kusaini mkataba huo, mkurugenzi Mkuu wa TTCL Waziri Waziri Kindamba amesema kuwa TTCL itapeleka mawasiliano kwenye kata 60 katika mradi wa awamu hii ya tatu ambapo jumla ya vijiji 141 vitanufaika na mradi huu wa TTCL ambapo jumla ya wanakijiji wasiopungua laki sita watanufaika. Ameongeza kuwa TTCL tutatekeleza mkataba huu kwa kasi na kwa viwango  kama ambavyo Sheria iliyoanzisha TTCL inatutaka kupeleka mawasiliano kwa watanzania. “Tumejipanga kuhakikisha kuwa kila kona wananchi wanapata mawasiliano,” amesisitiza Kindamba


from MPEKUZI

Comments