Msajili Apangua Hoja za Vyama vya Siasa Kuhusu Muswada Mpya

Msajili wa Vyama Vya Siasa  amevitaka vyama vilivyoitisha mkutano wa kuupinga Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Vyama vyaSiasa kuacha propaganda za kupotosha muswada huo kwa sababu hatua zote za mchakato wa maboresho walishirikishwa.

Ametoa kauli hiyo siku moja baada ya kufanyika mkutano wa vyama 15 vya siasa ambavyo pamoja na mambo mengine,vilitangaza kuupinga hadharani Muswada wa Mabadiliko ya Sheria ya Vyama vya Siasa vikidai unatengeneza kaburi la vyama vya siasa na demokrasia nchini.

Akijibu hoja za viongozi wa vyama hivyo kwenye mahojiano yaliyofanyika  Dar es Salaam jana, Msajili Msaidizi wa vyamavya Siasa, Sisty Nyahoza alidai  kilichosemwa na viongozi hao ni upotoshaji na kutengeneza propaganda zauongo.

Alisema lengo la serikali katika sheria mpya ni kuhakikisha   vyama vya siasa nchini vinapata sheria bora inayokwenda na wakati ambayo itatoa nafuu kwa vyama vya siasa kuendesha shughuli zao kwa uhuru na kwa mujibu wa katiba za vyama vyao.

Alisema  hakuna kipengele ambacho kinampa mamlaka msajili kuingilia uamuzi wa ndani ya vyama vya siasa.

Kwa mujibu wa Msajili, ameshangazwa kusikia  marekebisho hayo yanakwenda kuua au kukandamiza vyama vya siasa wakati siyo kweli kwa sababu vyama hivyo vilitoa maoni yao wakati wa mchakato wa maoni mpaka hatua ilipofikia.

“Sasa kama wanaona muswada wa marekebisho ya sheria ya vyama vya siasa unakwenda kuua au kuvikandamiza vyama kwa nini walitoa maoni yao?.

“Kwa sababu tuliwashirikisha hatua zote pamoja na kuitisha mikutano ya kujadili, kama waliona kunà dosari kwa nini wasingesema mapema mpaka wamesubiri usomwe kwa mara ya kwanza bungeni.

“Waache unafiki,wasiwaaminishe wananchi kwa propaganda za uongo,” alisema Nyahoza.

Alisema  kilichofanyika kwenye muswada huo ni maboresho ya kawaida ambayo vyama na serikali wamekuwa wakifanya kwenye sheria au katiba zao  kuhakikisha wanapata sheria bora.

Alitoa mfano wa Chama Cha ACT-Wazalendo ambacho alisema kiliwahi kufanya marekebisho ya katiba yake, vivyo hivyo kwa msajili wa vyama vya siasa kufanya maboresho ya sheria zake.

Alisema hakuna kipengele ambacho kinaonyesha msajili anaweza kuingilia uamuzi wa vyama.

Alisisitiza hoja hiyo ni dhaifu kwa sababu kila chama kinaongozwa na katiba yake, hivyo  kuwaaminisha wananchi katika hoja hiyo ni kupotosha ukweli.

“Kwa mfano, sheria ya zamani inasema chama au mtu akifanya makosa iwe madogo au makubwa katika chama, chama hicho kifutwe,lakini muswada huu umesema chama au mtu katika chama akifanya makosa aonywe na msajili au kupewa adhabu ndogo ya kusimamisha kwa muda kutojihusisha na shughuli za siasa ama kulipa faini,” alisema.

Alisema katika muswada huo mpya hakuna kipengele kinachowazuia wanasiasa kuhama chama, kugombea   baada ya kuhama au kujiunga na vyama vingine, bali wanasiasa watafanya hivyo kwa mujibu wa katiba ya chama alichotoka au anachokwenda na   msajili hatahusika na lolote katika jambo hilo.

Alisema mpaka sasa  Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria bado inaendelea na mchakato wa kukusanya maoni.

Alisema kama wanaona kuna shida walipaswa kuwasilisha maoni yao na kuainisha vipengele ambavyo wanaona vina matatizo  viweze kufanyiwa marekebisho na siyo kuwadanganya wananchi kama walivyofanya.

Alisema kama wanadhani serikali ina nia ya kufuta vyama vyama vya upinzani au kuvikandamiza siyo kweli  kwa sababu serikali hiyo hiyo ndiyo iliyoanzisha mfumo wa vyama vingi mwaka 1992 baada ya kuona kuna umuhimu wa kuwapo   vyama hivyo.

Msajili wa vyama vya siasa ni mlezi wa vyama hivyo na   ataendelea kufanya shughuli zake kwa mujibu wa sheria na katiba na si vinginevyo,  alisema.

Aliwataka wanasiasa na wananchi kwa ujumla wao kuusoma muswada huo  waweze kuuelewa jambo ambalo linaweza kuepusha upotoshaji.


from MPEKUZI

Comments