Mpango Mkakati Wa Kitaifa Umeimarisha Wigo Wa Haki Za Binadamu

Na Ismail Ngayonga,MAELEZO
SERIKALI inao wajibu wa kulinda na kukuza Haki za Binadamu kama ilivyoelezwa na kufafanuliwa ndani ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Mikataba ya Kimataifa na Kikanda ya Haki za Binadamu na sheria mbalimbali za nchi.

Kwa kutimiza wajibu wa kulinda na kukuza Haki za Binadamu, Tanzania ni miongoni mwa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa zilizoridhia mikataba mingi ya kimataifa inayohusu Haki za Binadamu.

Miongoni mwa mikataba hiyo ni pamoja na Tamko la Ulimwengu juu ya Haki za Binadamu la 1948, Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa wa 1966, Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiuchumi, Kijamii na Kiutamaduni 1966, Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Watoto 1989, Mkataba wa Kimataifa wa Kuondoa aina zote za Ubaguzi wa mwaka 1965 n.k.

Aidha, pamoja na kuridhia mikataba hii, Serikali imekuwa ikiandaa ripoti mbalimbali za utekelezaji wa Haki za Binadamu ambazo zimekuwa zikiwasilishwa kwenye vyombo vya kimataifa kwa ajili ya kujadiliwa na kutolewa mapendekezo ya utekelezaji.

Katika kuhakikisha kuwa Tanzania inakuwa kinara wa kujali Haki za Binadamu, Serikali imeanzisha taasisi mbalimbali zinazoshughulikia masuala ya kulinda na kukuza haki nchini, ikiwemo Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora; Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi; Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU); Bunge na Mahakama.

Serikali pia imejenga mazingira mazuri na kuruhusu taasisi zisizo za kiserikali kuanzishwa kwa lengo la kusaidia juhudi zake za kuimarisha Haki za Binadamu hapa nchini, ambapo hadi sasa kuna takribani mashirika 5,000 yasiyo ya kiserikali yanayojihusisha na utetezi wa Haki za Binadamu.

Ili kuboresha mazingira ya upatikanaji na utoaji wa Haki za Binadamu nchini, Serikali imeendelea kuweka misingi imara ya kuhakikisha kuwa wananchi wote hasa wale wa kawaida, wanapata msaada wa kisheria kwa kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo Kuanzisha mchakato wa kuwa na Sekretarieti ya Huduma za Kisheria.

Akiwasilisha Makadirio ya Hotuba ya Bajeti kwa mwaka 2018/19, Waziri wa Katiba na Sheria, Prof. Palamagamba Kabudi anasema  katika Mwaka wa Fedha 2017/2018 Wizara iliendelea kuimarisha na kusimamia haki za binadamu kama zilivyoainishwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na sheria za nchi.

Anaongeza kuwa katika kipindi hicho, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali iliratibu maandalizi ya Rasimu ya Taarifa ya Nchi ya Utekelezaji wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Watu Wenye Ulemavu wa Mwaka 2009 na pia kutoa mafunzo kwa maafisa wa Serikali wakiwemo Mawakili wa Serikali kuhusu masuala ya haki za binadamu na biashara yaliyofanyika Bagamoyo, Pwani mwezi Agosti, 2017.

Prof. Kabudi anasema Serikali iliendelea kuiwezesha Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ili iweze kutekeleza majukumu yake ya msingi ya kufuatilia na kutoa ushauri kwa Serikali na taasisi zake kuhusu utekelezaji wa Haki za Binadamu na misingi ya utawala bora nchini.

Akifafanua zaidi anasema Kutokana na juhudi hizo za pamoja (kati ya Serikali na Tume), Tume imefanikiwa kupata Daraja la “A” baada ya kufanyiwa Tathmini na Mtandao wa Tume za Haki za Binadamu Duniani, ambapo mafanikio hayo kielelezo dhahiri kuwa nchi Serikali inaheshimu na kuzingatia haki za binadamu.

Kwa mujibu wa Prof. Kabudi anasema Serikali kupitia Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora imeendelea kufuatilia haki za binadamu kwa watu walio katika makundi yenye mahitaji maalum, mahabusu na wafungwa; na kufanya uchunguzi wa malalamiko ya uvunjwaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora.

“Katika kipindi cha kuishia mwezi Machi, 2018, Tume ilifanya ukaguzi katika magereza 28 na vituo vya polisi 21 katika mikoa ya Ruvuma, Njombe, Geita, Kagera, Simiyu, Shinyanga, Morogoro na Dodoma na kukagua taasisi ya Isanga inayohifadhi wagonjwa wa maradhi ya akili ambao awali walishtakiwa kwa kutenda makosa ya jinai wakiwa na maradhi ya akili” anasema Prof Kabudi.

Waziri Kabudi anasema Tume pia ilishughulikia malalamiko ya uvunjifu wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora ambapo kufikia Machi, 2018 ilipokea malalamiko mapya 431 na kufanya jumla ya malalamiko kuwa 7,055, ambapo malalamiko 412 yamefanyiwa uchunguzi na kuhitimishwa na mengine 6,610 yanaendelea kuchunguzwa.

Anasema Tume pia ilifanya uchunguzi wa hadhara wa migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji; na wananchi na wawekezaji katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Singida na Manyara na kuwasilisha mapendekezo yake kwa taasisi zinazohusika na migogoro hiyo.

Prof Kabudi anasema  katika Mwaka wa Fedha 2017/2018, Serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi ya upatikanaji wa huduma ya msaada wa kisheria nchini na kuandaa Kanuni za Sheria ya Msaada wa Kisheria zilizotangazwa katika Tangazo la Serikali Na. 44 la tarehe 9 Februari, 2018 na kufanya uteuzi wa Msajili wa Watoa Huduma ya Msaada wa Kisheria.

“Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, TAMISEMI imekamilisha uteuzi wa Wasajili Wasaidizi wa watoa huduma ya msaada wa kisheria ngazi ya mikoa na wilaya Tanzania Bara. Mafunzo kwa ajili ya Wasajili hao yameanza kutolewa mwezi Aprili, 2018 ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi” anasema Prof Kabudi.

Usimamizi wa Haki za Binadamu na ujenzi wa Maadili mema ndani ya jamii yetu, ni jukumu la kila mmoja wetu, kila mmoja  kwa namna moja au nyingine anawajibu wa kulinda, kuheshimu na kudumisha Haki za Binadamu.


from MPEKUZI

Comments