Mahakama Yakubali Aliyefoji Saini ya Wazir Makamba Akahojiwe TAKUKURU

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeruhusu,Magori Wambura mshtakiwa wa kwanza katika kesi ya kughushi saini ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Januari  Makamba,  kwenda kuhojiwa na Takukuru.

Wambura ambaye ni ofisa mazingira  kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na wenzake watano wanakabiliwa na mashtaka sita yakiwemo ya kula njama na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Uamuzi huo umetolewa leo Ijumaa Desemba 14, 2018 na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Augustina Mmbando baada ya upande wa mashtaka kuiomba mahakama hiyo  kumhoji mshtakiwa huyo.

Wakili kutoka Takukuru, Leonard Swai ameieleza mahakama hiyo kuwa wanaomba kibali cha kumhoji mshtakiwa huyo kwa makosa mengine.

Baada ya Swai kutoa maelezo hayo, Hakimu Mmbando alikubaliana na upande wa mashtaka na kuruhusu Wambura kwenda kuhojiwa.

"Mahakama imekubali Wambura ahojiwe lakini wakati anahojiwa wakili wake anaruhusiwa kushiriki katika mahojiano hayo,” amesema hakimu Mmbando.

Hakimu Mmbando baada ya kueleza hayo ameahirisha  kesi hadi Desemba 19, 2018 itakapotajwa.

Wambura anatetewa na wakili Ntumika Godfrey na yupo  rumande katika gereza la Segerea baada ya kukosa dhamana.


from MPEKUZI

Comments