Waziri wa Fedha : Sina taarifa ya taasisi iliyositisha mikopo Tanzania

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, amesema yeye kama waziri wa fedha hana taarifa yoyote ya taasisi ambayo imetishia kuacha kutoa mkopo ama msaada kwa Tanzania.

Dk. Mpango amesema hayo bungeni jijini Dodoma leo Jumatano Novemba 14, alipokuwa akijibu hoja za wabunge walizotoa wakati wakichangia Azimio la Bunge la Mkataba wa Takwimu Afrika.

Wakati Dk Mpango akitamka hivyo, kumekuwa na taarifa kwenye vyombo vya nje ya nchi na mitandao ambavyo vimekuwa vikiripoti kuwa, Benki ya Dunia imesitisha mikopo katika sekta ya takwimu na elimu kwa sababu ya mambo mbalimbali ikiwamo Sheria ya Takwimu ya Mwaka 2015.

Wakati wa kuchangia mjadala huo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, ilisema kutokana na Sheria ya Takwimu ya mwaka 2015 na marekebisho yake ya 2018, yamekuwa yakifanya baadhi ya tasisi kutishia kuacha kutoa mikopo na misaada kwa Tanzania.

Pia ilisema Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari, zinawabana wanasiasa na kupewa kesi za uchochezi na kwamba hivi karibuni Dk. Mpango alipokutana na viongozi wa Benki ya Dunia alionyesha kulegeza mashari ya sheria hiyo.

Akijibu hoja hizo, Dk Mpango amesema; “kulikuwa na madai kuwa baadhi ya wadau wametishia kutoa fedha, mimi ndiyo Waziri wa Fedha na sijaona taarifa yoyote ya taasisi iliyoonyesha kuacha kutoa mkopo. Kuna taratibu za taasisi hizi kutoa taarifa na kote sijaona.

“Kuna taarifa pia kuwa mimi nililegeza masharti ya sheria hii nilipokutana na watu wa benki ya dunia. Ukweli ni kwamba mimi siwezi kulegeza sheria iliyopitishwa na Bunge, nilipokutana na Makamu Rais wa Benki ya Dunia nchini Indonesia nilimfafanulia malengo ya sheria hiyo na nikamwambia kama anaweza kutuma mwakilishi wao wakati tunatunga kanuni za sheria hii,”.

Kuhusu hoja ya upinzani kuwa, Sheria ya Takwimu na ile ya makosa ya mtandao kwamba imekuwa mwiba kwa vyombo vya habari na hivyo ibadilishwe, Dk Mpango amesema;  “sheria hizi pengine ni mwiba kwa vyombo vya habari vinavyovunja sheria siyo vinginevyo.

“Na kusema Sheria ya Huduma kwa vyombo vya habri ni mwiba kwa wanasiasa, niseme tu wanaotumia takwimu za mfukoni au za uongo, wataendelea kupata tabu sana tu, tunaomba wafuate sheria,”.

Kuhusu hoja ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kutotoa taarifa za fedha kwa wakati, Dk. Mpango amesema taarifa za chombo hicho hutolewa kwa wakati labda pale tu kunapokuwa na sababu maalumu.

Amesema pia Tanzania ilisaini mkataba huo na kukaa kwa miaka tisa bila kuridhia tamko hilo kwa sababu ilikuwa lazima kwanza sheria ya takwimu itungwe.


from MPEKUZI

Comments