Waziri Mkuu: Maonesho Ya Viwanda, Biashara Na Madini Yanapaswa Kuigwa Na Mikoa Mingine

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema maonesho ya viwanda vidogo na biashara ndogondogo pamoja na yale ya teknolojia na uwekezaji katika sekta ya madini yanayofanyika nchini ni ubunifu muhimu na hauna budi kuigwa na mikoa mingine.

“Ubunifu huu wa kufanya maonesho ya viwanda ya kimkoa, kikanda na kitaifa ni jambo muhimu sana. Maonesho haya, yanatupa fursa ya kujitangaza na kutathmini hatua tuliyofikia katika utekelezaji wa ajenda ya ujenzi wa uchumi wa viwanda na kubaini changamoto zilizopo,” amesema.

Akizungumza wakati akitoa hoja ya kuahirisha mkutano wa 13 wa Bunge leo (Ijumaa, Novemba 16, 2018) bungeni mjini Dodoma, Waziri Mkuu amesema maonesho hayo yanahamasisha wananchi wengi zaidi washiriki kwenye ujenzi wa uchumi wa viwanda.

“Napenda kuielekeza mikoa mingine iige mifano hiyo ya mikoa ya Pwani, Simiyu na Geita ili kuhamasisha wananchi na wadau wengine washiriki ipasavyo katika ujenzi wa viwanda na kuleta teknolojia mpya za viwanda na sekta ya madini,” amesema.

Amesema mbali ya kujifunza teknolojia mpya, maonesho hayo yanatoa fursa kwa wadau husika kukutana na kubadilishana utaalam na uzoefu mbalimbali.

“Napenda nitumie fursa hii kuwapongeza Wakuu wa Mikoa ya Pwani, Simiyu na Geita kwa ubunifu wao huo. Vilevile, niwapongeze sana wazalishaji wenye viwanda na madini pamoja na wadau wote walioshiriki kuonesha teknolojia mbalimbali na bidhaa mpya za kilimo na madini katika maonesho hayo.”

Amesema kupitia maonesho hayo, wachimbaji hao wadogo, pia waliweza kukutana na wataalamu wanaosimamia sekta ya madini na mabenki kwa lengo la kujifunza matumizi ya teknolojia mpya sambamba na kufahamu taratibu mbalimbali za kupata mikopo ya kuendesha shughuli zao za uchimbaji madini.

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwataka wananchi wajenge utamaduni wa kutumia bidhaa zinazozalishwa nchini ili kulinda viwanda vya ndani na kukuza uchumi.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Tanzania inakabiliwa na changamoto kubwa ya uharibifu wa mazingira na vyanzo vya maji na kwamba hatua stahiki hazina budi kuchukuliwa ili kudhibiti hali hiyo isiendelee.

Akitoa mfano Waziri Mkuu amesema: “Miradi mingi ya maji nchini imekwama au kutoleta tija kutokana na uharibifu wa mazingira na vyanzo vya maji. Hivyo, niwasihi Wabunge wenzangu muwahamasishe wananchi na wadau kutoa maoni yatakayosaidia kujenga na kuboresha vema sheria zinazokusudiwa kulinda mazingira yetu pamoja na vyanzo vya maji.”

Hata hivyo, Waziri Mkuu amebainisha faraja aliyoipata wakati alipofanya ziara ya kikazi wilayani Lushoto na kukuta mazingira yametunzwa vizuri na uoto wa asili umehifadhiwa, na akaagiza Halmashauri nyingine ziige mfano huo wa utunzaji mazingira.

“Katika ziara yangu ya hivi karibuni wilayani Lushoto, nilifarijika mno kuona jitihada kubwa zinazofanywa na wananchi wa wilaya hiyo katika kuhifadhi mazingira. Nitumie fursa hii kuwapongeza wananchi wa Halmashauri za Wilaya ya Lushoto na Bumbuli kwa utunzaji mzuri wa mazingira. Naziagiza Halmashauri nyingine nchini ziige mfano huo mzuri wa kuhifadhi mazingira,” amesema.

Bunge limeahirishwa hadi Januari 29, mwakani.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
IJUMAA, NOVEMBA 16, 2018.


from MPEKUZI

Comments