Vikundi Vya Upatu Kutosimamiwa Na Sheria Mpya Huduma Ndogo Za Fedha

Na Farida Ramadhani, WFM, Dodoma
Serikali imesema kuwa vikundi vya Upatu havitasimamiwa chini ya Sheria mpya ya Huduma Ndogo za Fedha ya Mwaka 2018 (The Microfinance Act, 2018) kwa sababu havijihusishi na biashara ya huduma ndogo za fedha.

Hayo yameelezwa bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) wakati akihitimisha hoja za mjadala wa Muswada wa Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya Mwaka 2018.

Dkt. Mpango alisema Sheria hiyo itahusisha taasisi kama vile Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo (SACCOS), Taassi za huduma ndogo za fedha zisizopokea na zinazopokea amana na vikundi vya kifedha vya kijamii, wakopeshaji binafsi na asasi za kijamii.

Alieleza kuwa Sheria hiyo pia inalenga kuwalinda wananchi wanaotegemea sekta ndogo ya fedha katika kuendesha maisha yao na shughuli za kiuchumi kwa ujumla na itasimamia na kudhibiti biashara ya huduma ndogo za fedha, kuwawezesha watumiaji na watoa huduma hiyo pamoja na kudhibiti changamoto zinazoweza kutokea katika sekta hiyo.

“Madhumuni ya Sheria hiyo ni kuwatambua watoa huduma ndogo za fedha kwa lengo la kuwasimamia, kupata takwimu, kuwalinda na kuwawezesha watumiaji wa huduma ndogo za fedha”,  alisema Waziri Mpango.

Dkt. Mpango aliongeza kuwa Sheria hiyo imeweka utaratibu wa kuiwezesha Benki Kuu kutoa elimu kwa watumiaji wa huduma ndogo za fedha hususan vikundi vya kijamii kwa lengo la kunufaika na fursa zilizopo.

Aliongeza kuwa wakati Benki Kuu itakapolazimika kusimamia Taasisi za huduma ndogo za fedha, taasisi hizo  hazitatozwa fedha kugharamia majukumu ya Benki Kuu.

Akizungumzia maoni wa wabunge kuhusu daraja la nne la Sheria hiyo linalohusu vikundi vya kifedha vya kijamii, wakopeshaji binafsi na asasi za kijamii, Waziri Mpango alifafafanua kuwa Sheria hii imebainisha kwamba kutaandaliwa kanuni na miongozo mahsusi kwa ajili ya kusimamia daraja hilo.

“Sheria hii inaainisha shughuli mbalimbali zinazoweza kufanywa na mabenki na taasisi za fedha zinazoweza kusaidia katika kulea na kukuza watoa huduma wa daraja la nne. Miongoni mwa shughuli hizo ni pamoja na utoaji mikopo yenye msharti nafuu na elimu ya fedha”, alisema Dkt. Mpango.

Alisema kuwa Serikali imejipanga kutenga fedha kwa ajili ya utekelezaji wa usimamizi wa daraja la nne. Mwongozo kwa ajili ya maandalizi ya bajeti ya 2019/20 umetoa maelekezo kwa Halmashauri zote kutenga fedha kwa ajili ya kazi hii.

Aidha, baada ya Waziri Mpango kuwasilisha hoja hizo, Bunge lilipitisha Muswada wa Sheria hiyo ambao umeundwa baada ya kujitokeza changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ndogo ya fedha ikiwemo Taasisi za huduma ndogo za fedha kutoa mikopo kwa wananchi kwa vigezo na masharti magumu na hivyo kusababisha madhara kwa wananchi ikiwemo mali zao kuuzwa pasipo kufuatwa kwa taratibu za kisheria.

Mwisho


from MPEKUZI

Comments