Uganda yaisafishia njia Taifa Stars AFCON.....Ikiichapa Lesotho leo, safari ya Cameroon imeiva

Wakati macho na masikio ya mashabiki, wadau wa soka na Watanzania kwa ujumla, leo wakiyaelekeza nchini Lesotho kwenye mechi ya kuwania kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika kati timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' na wenyeji wa mchezo huo, Lethoto, Uganda imekisafishia njia kikosi hicho cha Emmanuel Amunike baada ya kuichapa Cape Verde jana.

Uganda ambayo ipo Kundi L pamoja na Taifa Stars na Lesotho, jana ilikuwa mwenyeji wa Cape Verde katika kinyang'anyiro hicho cha kuwania kufuzu fainali hizo zitakazofanyika Cameroon mwakani na kufanikiwa kuibuka na ushindi wa bao 1-0.

Lilikuwa bao la dakika ya 78 lililotiwa kambani kwa kichwa na straika Patrick Kaddu na hivyo kuifanya Uganda kufikisha pointi 13 hivyo kufuzu moja kwa moja fainali hizo huku ikiwa na mechi moja mkononi.

Kwa matokeo hayo ya Uganda, kama Stars leo itashinda itafikisha pointi nane, na moja kwa moja itaungana na Waganda hao katika fainali hizo za mwakani kwani katika kundi lao hakuna timu nyingine inayoweza kuzifikisha pointi nane.

Ikumbukwe kila timu imebakiza mechi moja, jambo ambalo kama Cape Verde itashinda mechi yake ya mwisho itafikisha pointi saba, wakati Lesotho ikipoteza leo dhidi ya Stars na kisha kushinda mechi ya mwisho ugenini kwa Cape Verde itafikisha pointi tano.

Lakini pia kama Stars itatoka sare italazimika kushinda mechi ya mwisho nyumbani dhidi ya Uganda kwani sare yoyote inaweza kuigharimu endapo Cape Verde mchezo wake wa mwisho itaifunga Lesotho.

Matokeo kama hayo yatazifanya Stars na Cape Verde kulingana pointi kila moja ikifikisha saba, hivyo kutegemea sasa kubebwa kwa tofauti nzuri ya mabao ya kufunga na kufungwa.

Kazi moja kwa Stars leo, ni ushindi tu ili kuweza kufuzu na mechi ya mwisho dhidi ya Uganda kila moja kucheza kwa kujifurahisha kwani zitakuwa zote zimeshafuzu. Hiyo ni kutokana na Stars hadi sasa kubaki nafasi ya pili ikiwa na pointi tano, ikifuatiwa na Cape Verde yenye pointi nne huku Lesotho ikiwa na pointi mbili kabla mechi yao ya leo.

Katika mchezo wa leo Stars inayohitaji ushindi leo, itawakosa nahodha wake Mbwana Samatta ambaye ana adhabu ya kadi mbili za njano na Shomari Kapombe ambaye ni majeruhi.

Nafasi ya Kapombe inatarajiwa kuzibwa na beki wa Nkana Rangers, Hassan Kessy huku John Bocco akitarajiwa kuanza kwenye nafasi ya Samatta.


from MPEKUZI

Comments