Swali la Kwanza la Charles Mwijage Bungeni Tangu Atumbuliwe Uwaziri

Aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Charles Mwijage ameibuka na kuzungumza bungeni, kwa mara ya kwanza tangu atenguliwe nafasi yake na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli wiki iliyopita.
 
Akizungumza Bungeni Jijini Dodoma kabla hajauliza swali kwa Wizara ya Nishati, Mwijage amelishukuru bunge hilo kupitia kwa Spika Job Ndugai wakati wote wa Uwaziri wake ndani ya Bunge, akisema,

“Nawashukru sana tangu mlivyokuwa mkiniongoza bungeni, kupitia kwako Mwenyekiti napenda kumshukuru Rais,  Makamu wa Rais na Waziri Mkuu kwa namna ambavyo waliniamini na kunisimamia kwenye majukumu ambayo waliyonipa."

Mbunge huyo huku akishangiliwa, alisema wananchi wake walipata mradi wa umeme katika jimbo zima lakini maeneo mengi yaliishia kuwekwa mambo bila ya kusimikwa kwa nguzo.

"Ni lini sasa Serikali itawaondolea kero ya umeme ili wananchi wale nao waanze kunufaika na miradi ya Rea," alisema Mwijage

Akijibu swali hilo, Waziri wa Nishati,  Dk  Medard Kalemani alisema miradi ya umeme katika wilaya ya Muleba itatekelezwa muda si mrefu na mkandarasi yuko katika maandalizi ya kupeleka nguzo.


from MPEKUZI

Comments