Rais Magufuli Kufungua Mkutano Wa 21 Baraza La Mawaziri Nchi Wanachama Wa Mto Nile

Rais John Magufuli, anatarajia kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa mkutano wa 21 wa Baraza la Mawaziri wa Maji katika nchi wanachama Bonde la Mto Nile zilizoko kwenye ukanda wa Maziwa Makuu (NESLAP).

Katika mkutano huo utakaofanyika Novemba 22, mwaka huu, jijini Dar es Salaam, baadhi ya mambo yatakayojadiliwa ni pamoja na kupitia utekelezaji wa masuala mbalimbali ya miradi, kupokea taarifa ya utendaji, hali ya ulipaji wa michango ya mwaka kwa kila nchi mwanachama na tathmini ya watumishi wa sekretarieti ya NELSAP.

Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Prof. Makame Mbarawa, alisema jana jijini hapa kuwa, Tanzania inatarajiwa kuwa mwenyeji wa mkutano huo ambao ni wa kawaida wa kiutendaji.

"Baraza la mawaziri wa maji ndicho chombo cha juu kabisa cha uamuzi katika kusimamia na kuendesha shughuli za bonde la Mto Nile katika ukanda wa Maziwa Makuu na mkutano huu ufanyika mara moja kila mwaka kufuata mzunguko katika nchi wanachama," alisema Prof. Mbarawa.

Aidha, alisema mkutano huo utatanguliwa na vikao vya wataalamu vitakavyoanza Novemba 20 hadi 21, jijini Dar es Salaam.
 
"Vikao hivyo vya wataalam ambavyo ni vya kiutendaji hufanyika mara mbili kwa mwaka kufuata mzunguko katika nchi wanachama," alisema Prof Mbarawa.

Aliongeza kuwa, ushirikiano wa nchi za bonde la Mto Nile ni wa muda mrefu ambao ulianza tangu mwaka 1960 na ilipofika Februari 22, 1999 nchi wanachama ziliunda taasisi ya mpito iitwayo Nile Basin Initiative (NBI0).

"Malengo ya ushirikiano huu ni kufikia uanzishwaji wa kamisheni ya Bonde la Mto Nile ambayo mchakato wake unaendelea" alisema Prof. Mbarawa.

Aliongeza kuwa, Tanzania ni miongoni mwa nchi 11 za Bonde la Mto Nile zinazoshirikiana katika kusimamia na kuendeleza rasilimali za bonde la mto huo chini ya mwavuli wa NBI.

Alizitaja nchi zingine kuwa ni Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Misri, Ethiopia, Kenya, Rwanda, Sudani Kusini, Sudan, Uganda na Eritrea ambayo ni mtazamaji.

Alisema ushirikiano huo una faida kubwa na nchi wanachama zinanufaika na maji ya Mto Nile kwa kuwa na haki sawa ya matumizi.
 
Hata hivyo, alisema katika mkutano huo, Tanzania ambayo ndiyo mwenyekiti kwa sasa itakabidhi kijiti hicho kwa Uganda.



from MPEKUZI

Comments