Mchungaji Msigwa atolewa bungeni Mjadala wa Kumpongeza Rais Magufuli Ukiendelea

Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (Chadema), ametolewa nje ya ukumbi wa Bunge, wakati Bunge likijadili azimilio lililowasilishwa bungeni na Mbunge wa Singida Magharibi (CCM), Elibariki Kingu, la kumpongeza Rais John Magufulu kwa hatua aliyochukua juu ya kununua zao korosho.

Chanzo cha kutolewa nje Msigwa ilikuwa ni mchango wa Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Jackline Ngonyani, ambaye alikuwa akichangia azimio hilo huku akiwaponda wapinzani.

Katika mchango wake alisema wapinzani wamekuwa mabingwa wa kupinga kila kitu kuanzia suala la makinikia na hata Mradi wa Umeme wa Mto Rufiji.

“Wakati wa suala la makinikia wapo tuliokuwa tunawaona wanazunguka hotelini huko kupanga mikakati ya kukwamisha, hoja ya kutengeneza umeme wa Mto Rufiji pia walipinga,” amesema.

Wakati Ngonyani akisema hayo, Msigwa alisimama akawa anazungumza jambo lililofanya Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson, kumtaka akae bila mafanikio.

“Msigwa wewe ni mchungaji, unajua kabisa Biblia inasema tuheshimu mamlaka mimi nazungumza wewe keti,” alisema.

Baada ya kujaribu kumsihi kwa muda bila mafanikio, alimuamuru kutoka nje, na alipokataa aliagiza askari wa bunge kumtoa nje.


from MPEKUZI

Comments