Waziri Ndalichako Amfananisha Rais Magufuli na Mwalimu Nyerere

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako amemfananisha Rais John Magufuli na Hayati Mwalimu Julius Nyerere akisema amekuwa mstari wa mbele kupigania masilahi ya Taifa na kupambana na viongozi wanaokwenda kinyume na matarajio ya Watanzania.

Akizungumza leo Oktoba 10, 2018 katika kongamano la kumuenzi Mwalimu Julius Nyerere linalofanyika katika Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Kigamboni Dar es Salaam, Profesa Ndalichako aliyekuwa mgeni rasmi amesema Mwalimu alijali masilahi ya Taifa na ndiyo maana hakuwa na mali nyingi hadi alipostaafu.

 “Mwalimu Nyerere alikuwa kiongozi wa mfano ambaye katika maisha yake aliweka mbele masilahi ya Taifa kuliko masilahi yake binafsi.”

“Tumeona hata wakati anastaafu ukiangalia mali alizokuwa nazo zilikuwa haziakisi nafasi ya uongozi katika Taifa aliyokuwa nayo katika miaka mingi ya uongozi,” amesema Profesa Ndalichako.

Amesema Mwalimu Nyerere hakuwa kiongozi aliyejinufaisha mwenyewe binafsi, bali alikuwa ni utumishi wa kuwatumikia Watanzania na alifanya kazi hiyo kwa uadilifu mkubwa na kwa unyenyekevu.

“Leo miaka 19 hatunaye Mwalimu Julius Kambarage Nyerere sote tunapaswa kumuenzi kwa kuiga mambo aliyofanya kwa Taifa,” amesema.

“Pia, tunashuhudia Rais wetu wa Awamu ya Tano, John Magufuli anavyoweka mbele masilahi ya Taifa na amekuwa mstari wa mbele katika kupigania rasilimali za Taifa na hana mchezo kabisa na yeyote anayekwenda kinyume na maadili ya Kitanzania.”

Profesa Ndalichako amewataka Watanzania kuendelea kumuunga mkono Rais Magufuli kwa kuwa ni mwepesi kuchukua hatua pale anapoona viongozi wa umma hawaendani na matarajio ya wananchi waliompa ridhaa ya uongozi.

Kongamano hilo lenye kauli ya ‘Falsafa ya Mwalimu Nyerere katika kujitegemea na maendeleo ya viwanda Tanzania, limehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally.

Wengine ni; Balozi Ibrahim Kaduma, aliyewahi kuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh, Jaji Mkuu mstaafu, Augustino Ramadhani na mwanasiasa mkongwe, Paul Kimiti na wengineo.

Akizungumzia utendaji wa Serikali, Profesa Ndalichako amesema Serikali imeendelea kutekeleza miradi ya maendeleo ikiwa ni pamoja na utoaji elimu bure, ujenzi wa viwanda na miundombinu ya uchukuzi kama kuimarisha shirika la ndege na ujenzi wa reli ya kisasa.

Ameendelea kusema Serikali imekuwa ikitekeleza mradi wa umeme wa Stieglier’s Gorge huku usambazaji wa umeme ukiendelea kwa kasi.


from MPEKUZI

Comments