Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aagiza mtumishi TRA kusimamishwa kazi

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Kagera kusimamishwa kazi ofisa wa mamlaka hiyo, Victor Mtei anayedaiwa kuvujisha mapato katika mpaka ya Mutukula na Murongo.

Ametoa agizo hilo leo Jumanne Oktoba 9, 2018 mjini Bukoba wakati akifanya majumuisho ya ziara yake ya kikazi ya  siku nne mkoani Kagera

Amesema ofisa huyo amekuwa akibadilishwa vituo vya mpakani pamoja na kudaiwa kushindwa kukusanya mapato huku akimtuhumu kupokea rushwa ya Sh 2 milioni.

Waziri Mkuu amesema baadhi ya maofisa wa TRA wanahusika na kuruhusu kuvushwa kwa kahawa za magendo kupitia mipaka iliyopo Wilaya za Missenyi, Karagwe na Kyerwa na kuagiza ofisa huyo asimamishwe.

Meneja wa TRA Mkoa wa Kagera, Adam Ntoga amesema ofisa huyo alikuwa tayari ameondolewa kituo cha Mutukula baada ya kutoridhika na utendaji wake na kuhamishiwa kituo cha Murongo Wilayani Kyerwa.

Waziri Mkuu amemuagiza Ntoga, kumsimamisha mara moja huku akionya kuwa uchunguzi zaidi unakuja dhidi ya viongozi wenye dhamana kujihusisha na mtandao wa magendo ya kahawa.


from MPEKUZI

Comments