Waziri Mkuu Atoa Siku Mbili Kwa Afisa Elimu Muleba

* Ifikapo Jumatano awe amepeleka walimu shule ya msingi Rwenzige
*Ina wanafunzi 216 wa darasa la awali hadi la nne bila mwalimu


 WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa siku mbili kwa Kaimu Afisa Elimu (Msingi) wa wilaya ya Muleba, mkoani Kagera Bw. Bukuru Malembo awe amepeleka walimu wawili katika shule ya msingi iliyoko kwenye kitongoji cha Rwenzige kwa kuwa haina mwalimu hata mmoja.

Shule hiyo yenye madarasa wawili na ofisi moja ya mwalimu ina jumla wanafunzi 216 wa darasa la awali hadi la nne, ilijengwa na wananchi ambapo wanafunzi wake wanafundishwa na mwananchi mmoja aliyemua kujitolea ili kuwapunguzia watoto kutembea umbali wa kilomita 16 kwenda kusoma katika shule ya kijiji cha Kiteme.

Waziri Mkuu alitoa agizo hilo jana (Jumatatu, Oktoba 8, 2018) baada ya wanafunzi wa shule hiyo kuwasilisha malalamiko yao kwa njia ya bango wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye kiwanja cha kituo cha afya Kimeya, baada ya kukagua majengo ya kituo hicho.

“Haiwezekani watoto wadogo wenye umri wa kuanzia miaka mitano wakatembea umbali wa kilomita 16 kwenda shule wakati katika kitongoji chao kuna shule yenye madarasa mawili na chumba kimoja cha ofisi ya mwalimu na Afisa Elimu hadi sasa hajapeleka walimu na kumuachia mwalimu Benson (kijana ambaye si mwalimu ila anajitolea kufundisha) akifundisha wanafunzi hao peke yake.”

Waziri Mkuu alimuagiza Afisa Elimu huyo ahakikishe ifikapo Jumatano (Oktoba 10, 2018) saa nne asubuhi awe ameshawapeleka walimu hao katika shule hiyo ya msingi ili waweze kuwafundisha wanafunzi hao na kisha Mkuu wa wilaya hiyo, Mhandisi Richard Ruyango awasilishe taarifa ya utekelezaji wa agizo hilo ofisini kwake. “Walimu wengi mmewaacha katika shule za barabarani huku za vijijini zikiwa hazina walimu.”

Kwa upande wake, Bw. Benson Bukerebe (29) maarufu mwalimu Benson alisema yeye kitaaluma si mwalimu bali ni mhitimu wa kidato cha nne, alimua kuanzisha darasa kwa ajili ya kuwafundisha wanafunzi hao kwani alikuwa akiwahurumia kwa sababu baadhi yao hawakuwa na uwezo wa kutembea umbali wa kilomita 16 hadi iliko shule ya msingi ya Kiteme.

Kijana huyo alisema kwa muda wote huo ameweza kumudu kuwafundisha wanafunzi hao kwa kutumia vitabu vya kuazima kutoka shule mbalimbali za msingi, lengo ni kuhakikisha watoto wenye umri wa kuanza shule katika kitongoji chao wanapata fursa ya elimu ambayo ni haki yao ya msingi.

Katika hatua nyingine,Waziri Mkuualisema Serikali imeweka sheria kali ili kuwalinda watoto wa kike na wanatakiwa kuheshimiwa katika jamii kwa kuachwa waendelee na masomo yao bila ya usumbufu wa aina yoyote na atakayebainika kukatisha masomo yao atachukulia hatua kali za kisheria.

Alisema Serikali  itatoa adhabu kali ya kifungo cha miaka 30 jela kwa mtu atakayekatisha elimu ya mtoto wa kike iwe kwa kumuoa, kumpa ujauzo na hata ukikutwa naye nyumbani kwako na katika nyumba ya wageni.

“Tukikukuta na binti wa shule katika kona isiyoeleweka tunakukamata na kukuchukulia hatua za kisheria. Ole wenuvijana, mkibainika mmewapa mimba mabinti wanaosoma, adhabu yake ni miaka 30 jela.”

Waziri Mkuu alisema kwa wazazi au walezi watakaowaozesha watoto kike ambao bado ni wanafunzi na kwa upande wa wazazi watakaomsindikiza mtoto wao wa kiume kwenda kuoa mwanafunzi wote watachukuliwa hatua za kisheria.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMANNE, OKTOBA 9, 2018.


from MPEKUZI

Comments