Waziri Mkuu Atoa Siku 10 Kwa Mkurugenzi Wa Mpwapwa Awe ameshatoa fedha za mikopo kwa vijana, wanawake na walemavu

WAZIRI MKUU Kassim ametoa siku 10 kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Mpwapwa, Bw. Peter Swea awe ametoa fedha za mikopo kwa ajili ya vijana, wanawake na walemavu.

"Leo (jana) ni tarahe 10 nataka hadi ikifika tarehe 20 ya mwezi huu uwe umeshatoa fedha za mikopo kwa wanawake, vijana na walemavu. Habari za mpaka kikao kiridhie hayo ni mambo ya zamani na ndio maana ikatungwa sheria kwa ajili ya jambo hilo. "

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo jana (Jumatano, Oktoba 10, 2018) wakati akizungumza na wananchi wa kata ya Kibakwe wilayani Mpwapwa mara baada ya kukagua ujenzi wa Kituo cha Afya cha Kibakwe, akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Dodoma.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo baada ya Mkurugenzi huyo kumueleza kuwa bado hajatoa fedha kwa ajili ya mikopo hiyo ambazo alipaswa kuzitoa kila robo mwaka, akidai bado kikao cha kuidhinisha hakijakaa.

Amesema fedha hizo ambazo ni asilimia 10 ya mapato ya ndani yanayokusanywa kwenye halmashauri, ambapo anatakiwa kutumia asilimia nne kwa ajili ya mikopo ya wanawake, asilimia mikopo kwa ajili ya vijana na asilimia mbili zitolewe kwa walemavu.

Kadhalika,Waziri Mkuu amewaagiza watendaji wote wa vijiji kuainisha maeneo yote yenye misitu na vyanzo vya maji pamoja na kuwachukulia hatua kali watu wote watakaobainika kukata miti bila kibali.

Amesema mtu yeyote atakayebainika kukata miti bila kibali achukuliwe hatua kali kwa sababu wamekuwa wakisababisha ukosefu wa maji, ambapo wakandarasi wa maji kwenye wilaya hiyo wanapata changamoto ya kukosa maji kwenye maeneo mengo wakati awali  Mpwapwa awali ilikuwa na ardhi ya chepechepe.

"Nimepata habari, hapa Kibakwe watu wanakata miti ili kushindana ubavu wao wa kuishi. Nawaagiza watendaji wote wa vijiji kuainisha maeneo yenye vyanzo vya maji na misitu na muyalinde. Madiwani pia mnatakiwa kushiriki kukemea ukataji miti.”

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Bw. Jabir Shekimweli ameishukuru Serikali kwa kutenga sh. bilioni 1.4 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa vituo vitatu vya afya ambavyo ni Kibakwe, Mima na Pwaga.

Amesema miradi hiyo imesimamiwa vizuri na kamati za ujenzi kwenye kata na vijiji husika kama ambavyo muongozo ulivyoelekeza.

NayeMbunge wa Jimbo la Kibakwe, Bw. George Simbachawene amesema utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) umefanyika kwa mafanikio makubwa kwenye sekta ya afya, umeme na elimu.

Mbunge huyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, ameomba ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami kutoka Kongwa, Mpwapwa hadi Kibakwe, uharakishwe ili kuondoa adha ya miundombinu inayowakabili wananchi.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU


from MPEKUZI

Comments