Waraka wa Tundu Lissu Akipangua Hoja ya Katibu Mwenezi CCM, Humphrey Polepole

Hoja ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole ya kwamba wapinzani watakaoshindwa kujiunga na chama hicho mwaka huu wasubiri hadi uchaguzi mkuu ujao, imemuibua mbunge wa Singida Mashariki (Chadema) Tundu Lissu akihoji uhalali wa hamahama hiyo.

Jana Polepole aliandika katika ukurasa wake wa Twitter “Tumezingatia na tunaweka jitihada zetu zote katika kushughulika na utatuzi wa shida za watu wetu wa Tanzania. Mwaka 2018 ndio mwisho kwetu kufanya chaguzi ndogo za ubunge kwa wale wanaohama vyama vyao na kujiunga na CCM. Watakaoikosa round hii mbaki hukohuko tutakutana 2020,”.

Wakati Polepole akisema hayo, aliyekuwa mbunge wa Simanjiro (Chadema) James Ole Millya alitangaza kukihama Chadema na kujiunga na CCM akiwa mbunge wa saba wa upinzani kujiunga na chama tawala.

Kauli hiyo imewaibua wanasiasa mbalimbali wakipinga kile kilichosemwa na Polepole akiwamo Lissu ambaye yupo nchini Ubelgiji akiendelea na matibabu.

Katika waraka wake uliotolewa leo, Oktoba 8, Tundu Lissu amesema hamahama ya viongozi wa  Chadema haiwezi kukiua chama hicho kwa sababu wanaohama Chadema ni wageni na hawajashiriki katika kukijenga chama hicho kikuu cha upinzani nchini.

“Katibu Mwenezi wa CCM, Polepole, amesema kwamba mwisho wa 'kuunga mkono juhudi za Rais Magufuli za kuwaletea wananchi maendeleo' ni Desemba 2018. Kwa nini zuio hilo la CCM linalingana ama kukaribiana na zuio la kikatiba na kisheria kwa chaguzi za marudio?" Ameandika Lissu

“Je, hii ni bahati mbaya tu au kuna njama iliyofichwa kwenye hii ratiba ya CCM na ratiba iliyowekwa na Katiba na Sheria za Uchaguzi?,”Amesema.

Amesema licha ya wabunge hao kuhama, Chadema itabaki kuwa imara huku akiwataka Watanzania kufikiria kwa undani juu ya kwanini viongozi hao wanahama hasa kipindi hiki.

“Huu mjadala wa hama hama ya wabunge wa Chadema ni muhimu sana. Unahitaji kujadiliwa kwa tahadhari na kwa umakini, vitu ambavyo ni adimu katikati ya kelele na vumbi kubwa vilivyotokana na hama hama hii,” amesema.

Amesema wabunge wote wanaokihama Chadema hivi sasa ni wapya na wengi wao walijiunga na Chadema kutokana na vuguvugu la Lowassa kuhamia Chadema mwaka 2015.

“Baadhi, kama Dk Mollel wa Siha na Ole Kalanga wa Monduli, waliingia  Chadema na bungeni kutokana na wimbi la Lowassa la '15. Baadhi, kama Waitara, Ryoba na Ole Millya, wana muda mrefu Chadema lakini ni wabunge wapya,” ameandika Lissu.

Amehoji “Kwani kujiuzulu ubunge au udiwani wa Chadema na baadaye kugombea nafasi zile zile kwa CCM ni njia pekee ya kumuunga mkono Magufuli? Kumbuka, John Shibuda wa Chadema na John Cheyo wa UDP walikuwa wakiunga mkono jitihada za Rais Kikwete (Jakaya) lakini hawakuwahi kujiuzulu ubunge au uanachama wa vyama vyao.”

Amesema sababu inayotolewa na wabunge hao ya kuwapo kwa migogoro ndani ya vyama pinzani si ngeni lakini ameshangazwa na wimbi la wabunge hao kuhamia CCM.

Wabunge sita waliohamia CCM ni Maulid Mtulia (Kinondoni-Cuf),Dk Godwin Mollel (Siha-Chadema) Julius Kalanga (Monduli-Chadema), Mwita Waitara (Ukonga-Chadema), Zuberi Kuchauka (Liwale-CUF),  Marwa Chacha (Serengeti-Chadema) huku  Lazaro Nyalandu (Singida Kaskazini) akitoka CCM kwenda Chadema.


from MPEKUZI

Comments