Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo Oktoba 8 mwaka 2018 imeshindwa kuendelea kusikiliza kesi ya kutoa lugha chafu ya matusi dhidi ya Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Magufuli inayomkabili Mbunge wa Kawe, Halima Mdee kwa sababu shahidi wa upande wa mashtaka aliyetarajiwa kutoa ushahidi hakufika.
Wakili wa Serikali Mwandamizi Mwita amedai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba kuwa kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya kusikilizwa lakini shahidi hajafika leo.
Alidai shahidi waliyemtarajia kutoa ushahidi katika kesi hiyo, walimtumia wito lakini kwa bahati mbaya yupo nje ya Mkoa wa Dar es Salaam, aliiomba mahakama kuipangia tarehe nyingine kesi hiyo.
Hakimu Simba ameiahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 22, mwaka huu kwa ajili ya kuendelea kusikilizwa kwa ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashtaka.
Katika kesi hiyo tayari mashahidi watatu wa upande wa mashtaka wamekwishatoa ushahidi katika kesi hiyo akiwamo mkuu wa Kituo cha Polisi cha Urafiki, Mrakibu wa Polisi (SP) Batseba Kasanga.
Mdee anadaiwa, Julai 3,2017 katika ofisi za Chadema alitamka maneno dhidi ya Rais John Magufuli kuwa “anaongea hovyohovyo , anatakiwa afungwe breki” na kwamba kitendo ambacho kingeweza kusababisha uvunjifu wa amani.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment