Mtendaji wa Kijiji Ahukumiwa Miaka Miwili Jela

Mahakama ya wilaya ya Siha imemhukumu mtendaji wa kijiji cha Ngaritati, Dauson Mollel (63), kwenda jela miaka miwili au kulipa faini ya Sh1 milioni baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kutafuna michango ya wananchi Sh2.4 milioni.

Katika hukumu hiyo iliyosomwa Ijumaa Oktoba 5, 2018 na Hakimu Mfawidhi wa wilaya ya Siha, Jathmin Athman, mfungwa huyo ameamriwa kurejesha fedha hizo mara tu atakapomaliza kifungo chake.

Taarifa iliyotolewa na mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Holle Makungu, iliwaonya viongozi na watendaji wa vijiji kutojiingiza kukusanya michango kwa manufaa binafsi.

Upande wa mashitaka ukiongozwa na Wakili wa Takukuru, Rehema Mteta, umedai mshitakiwa alitenda makosa hayo mwaka 2007, na baada kutoroka hadi alipokamatwa na kufikishwa mahakamani Februari 23,2017.

Wakili Mteta amedai mwaka 2008, mtendaji huyo alikusanya fedha kutoka kwa wenyeviti wa vijiji mbalimbali, kwa ajili ya ujenzi wa hosteli ya wasichana katika shule ya sekondari ya Nuhu wilayani Siha.

Hata hivyo, badala ya kuiwasilisha kwa mwajiri wake ambaye ni Halmashauri ya wilaya ya Siha, mtendaji huyo anadaiwa kuzitumia fedha hizo kwa matumizi anayoyajua mwenyewe kinyume cha malengo yaliyokusudiwa.

Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Jathmin Athman amesema ushahidi uliotolewa na mashahidi sita wa upande wa mashitaka, umeweza kuithibitishia mahakama bila kuacha mashaka, kuwa mtendaji alitenda kosa hilo.

Hakimu huyo amesema ametoa adhabu hiyo ili iwe funzo kwa watumishi wengine wa umma, ambao wana tabia au kuwa na mawazo kama ya mshitakiwa, ya kujihusisha na ubadhirifu wa fedha za umma.

Mara baada ya kutolewa kwa hukumu hiyo, mkuu wa Takukuru mkoa Kilimanjaro, Holle Makungu aliwaonya watumishi wa umma kufanya kazi kwa uadilifu, akisema taasisi yake haitamuonea haya mtumishi yoyote anayejihusisha na vitendo vya ufisadi.


from MPEKUZI

Comments