Hatimaye TAKUKURU Yamtia Mbaroni Zacharia Hanspoppe

Baada ya kumsaka kwa muda mrefu, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imemkamata mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya klabu ya Simba, Zacharia Hanspoppe.

Takukuru imemkamata Hanspoppe baada ya kumtangaza katika vyombo vya habari na kumtaka aripoti katika ofisi zake ili kujibu tuhuma zinazomkabili.

Hanspoppe alikamatwa juzi baada ya kutua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), saa 8.59 mchana akitokea Dubai.

Akizungumzia kukamatwa kwa mfanyabiashara huyo maarufu, naibu mkurugenzi mkuu wa Takukuru, Brigedia Jenerali John Mbungo alisema, “Ni kweli amekamatwa, alikamatiwa uwanja wa ndege mara tu alipowasili.”

Alisema walipata taarifa kwamba Hanspoppe anakuja nchini na wakawasiliana na watendaji wa Idara ya Uhamiaji.

“Na vijana wetu wakawepo pale wanamsubiri na alipofika tu wakamkamata. Hanspoppe ataunganishwa moja kwa moja mahakamani kesho (leo).”

Pamoja na Hanspoppe mwingine aliyekuwa anatafutwa na Takukuru ni Franklin Lauwo ambaye naibu mkurugenzi huyo wa Takukuru alisema kuwa amekwishawasiliana nao na kudai atajisalimisha mwenyewe mara baada ya kurejea nchini akitokea Pakistan.


from MPEKUZI

Comments