CRDB yaeleza sababu kumpumzisha Dk. Charles Kimei kabla ya muda Kuisha

Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya CRDB, imeeleza sababu za kumpumzisha aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo, Dk. Charles Kimei kabla ya muda wake kumalizika kuwa ni vigumu kwa benki hiyo kuwa na wakurugenzi wawili kwa wakati mmoja.

Awali, bodi hiyo ilieleza kuwapo kwa kipindi cha mpito cha takribani miezi minane ambacho Mkurugenzi Mtendaji mpya aliyetambulishwa leo, Abdulmajid Nsekela, angefanya kazi na Dk. Kimei aliyemaliza muda wake.

Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Jumatano Oktoba 10, wakati wa kumtambulisha Mkurugenzi mpya wa benki hiyo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Ally Laay, amesema katika kikao walichokaa Oktoba 2 mwaka huu, walitafakari upya uamuzi wake huo na kupitisha maamuzi kuwa Dk. Kimei apumzike.

“Tuliamua Dk. Kimei apumzike na kumpisha Mkurugenzi Mtendaji mpya kwa kutilia maanani misingi ya utawala bora na maadili yetu ya kazi ingeleta ugumu kwa benki kuwa na wakurugenzi watendaji wawili kwa pamoja kwa kipindi kirefu,” amesema Laay.

Aidha, amesema Nsekela ni mbobevu na ana weledi wa kutosha katika masuala ya uongozi wa mabenki hivyo kutohitaji kushikwa mkono kwa muda mrefu kama ilivyoamuliwa hapo awali.

Kwa upande wake Nsekela, ameishukuru bodi hiyo kwa kujenga imani kubwa kwake na kuona anastahili kuchukua kijiti cha Dk. Kimei.

“Benki ya CRDB ni kubwa sana na inafanya vizuri kwa muda mrefu lakini ukubwa si tija kwa sababu huku mbele tuendako mkubwa na mdogo mnaweza kuwa sawa,” amesema Nsekela.


from MPEKUZI

Comments