CHADEMA Wapangua Tuhuma Za Mbunge Wao Aliyejiuzulu Leo na Kuhamia CCM

Baada ya Mbunge wa Jimbo la Ukerewe mkoani Mwanza kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Joseph Michael Mkundi kutangaza  kujiuzulu na kuomba kujiunga na Chama cha Mapinduzi (CCM) usiku wa jana Oktoba 10, CHADEMA wamekanusha tuhuma alizozitoa dhidi ya chama hicho.

Kupitia barua aliyomwandikia Spika wa Bunge Job Ndugai, Mkundi amesema kuwa amechukua uamuzi huo baadaya kutopatiwa ushirikiano na chama chake katika maafa ya kuzama kwa kivuko cha Mv. Nyerere kilichopelekea vifo vya watu zaidi ya 230.

Mkurugenzi wa Itikadi, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa CHADEMA, John Mrema amesema kuwa Mbunge huyo alipatiwa ushirikiano ikiwemo wabunge kuchanga michango na kufika kisiwani Ukara.

"Wabunge walitoa rambirambi zao pamoja na kufika kwenye eneo la tukio pamoja na baadhi ya viongozi labda yeye aseme kama alitaka nani na nani wafike huenda kuna watu alitaka wafike na hawakufanya hivyo", amesema Mrema.

Mrema ameongeza kuwa chama kimeshangazwa na tuhuma hizo na wamejaribu kumtafuta lakini hakupokea simu na baadae hakupatikana tena, na kusema kuwa wanamtakia kila la heri katika maisha yake mapya anayokwenda kuanza huko aendako.

Katika barua yake kwa Spika wa bunge ya kujiuzulu uwanachama wa chama chake cha zamani (CHADEMA) na kujiuzulu nafasi yake ya Udiwani na Ubunge, amedai kuwa Chama chake cha zamani (CHADEMA) kimepoteza heshima na utu baada ya kumtelekeza katika kipindi ambacho alihitaji msaada na ushirikiano kutoka kwenye chama hicho na uongozi wake katika kipindi cha msiba wa ajali ya Kivuko cha MV Nyerere, iliyotokea Septemba 20, 2018.


from MPEKUZI

Comments