Aliyekuwa Mkurugenzi wa Bandari Tanzania (TPA), Ephraim Mgawe na Wenzake Kortini Kwa Matumizi Mabaya Madaraka...Mgawe Kakosa Dhamana

Aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa zamani wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Ephraim Mgawe na wenzake watatu, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kujibu kesi ya uhujumu uchumi.

Mgawe na wenzake watatu wanakabiliwa na mashtaka matatu likiwemo la matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia Serikali hasara ya Sh.984.8 Milioni .

Pamoja na Mgawe, washtakiwa wengine ni Wajumbe wa Bodi ya Manunuzi ya TPA, Happiness Senkoro, Apolonia Mosha na Theophil Kimaro ambao kwa pamoja wamesomewa mashtaka yao, mbele ya Hakimu Hakimu Mkazi Mkuu Wilbard Mashauri.

Akiwasomea hati ya mashtaka leo Jumatano Oktoba 17, 2018, wakili wa Serikali Mwandamizi, Patrick Mwita amedai Septemba 28, 2010 katika ofisi za TPA zilizopo Ilala, Dar es Salaam, Mgawe akiwa mtumishi wa umma kama Mkurugenzi Mkuu na ofisa masulufu, alitumia madaraka yake vibaya.

Amesema alishuhudia mikataba kati ya mamlaka hiyo na Kampuni ya Leighton Offshore Pte Ltd 19800397 na kupata faida ya Sh984,828,000 baada ya kuvunja sheria ya manunuzi kwa kuiwezesha kampuni hiyo kupata upendeleo.

Mwita amedai katika shtaka la pili la matumizi mabaya ya madaraka linalowakabili mshtakiwa wa pili, tatu na wa nne,  alidai kuwa Julai 13, 2010 katika ofisi ya TPA washtakiwa wakiwa watumishi wa umma na wajumbe wa bodi ya manunuzi, walitumia vibaya madaraka kwa kuidhinisha zabuni na kuvunja sheria ya manunuzi ya umma kwa kuiwezesha Kampuni ya Leighton Offshore Pte Ltd kupata faida ya Sh984,828,000.

Katika shtaka la tatu linalowakabili washtakiwa wote, inadaiwa kati ya Julai 13, 2010 na Juni 30, 2016 katika ofisi za mamlaka hiyo, washtakiwa wote wanne waliisababishia TPA  hasara ya Sh984,828,000.

Washtakiwa baada ya kusomewa mashtaka yanayowakabili, walikana  mashtaka hayo.

Upande wa Jamhuri umedai upelelezi wa kesi hiyo umekamilika hivyo uliomba tarehe ya kutajwa kwa ajili ya kupanga tarehe ya kusikiliza maelezo ya awali.

Mwita amedai upande wa mashtaka hauna pingamizi la dhamana.

Hakimu Mashauri amewataka washtakiwa kuwa na wadhamini wawili wa kuaminiwa wenye barua na nakala za vitambulisho vya uraia watakaotia saini hati ya dhamana ya Sh15milioni.

Pia,  amewataka washtakiwa wawasilishe Sh100milioni taslimu au hati ya mali isiyohamishika yenye thamani hiyo ya fedha.

Hata hivyo, mshtakiwa wa pili na wa tatu walitimiza masharti ya dhamana huku Mgawe na mshitakiwa wanne wakipelekwa mahabusu hadi Oktoba 31, 2018 kesi itakapokuja kwa ajili ya kuwasomea maelezo ya awali washtakiwa hao.


from MPEKUZI

Comments