Tido aiambia mahakama mchakato wa kuitoa TBC analogia yalikuwa maelekezo ya Kikwete

Mkurugenzi Mkuu wa zamani wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Tido Mhando amedai mchakato wa kulitoa shirika hilo analogia kuingia kwenye digitali ulitokana na maelekezo ya Rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete.

Amedai hatua hiyo ilitokana na uamuzi wake wa kumtaka alibadilishe shirika lifikie katika hadhi inayostahili ambapo pia mchakato huo ulifanywa na Bodi ya shirika hilo na kupata baraka za Bodi ya Zabuni.


Tido anakabiliwa na mashtaka manne ya kutumia madaraka vibaya na moja la kuisababishia Serikali hasara ya Sh887.1 milioni.

Tido ameyaeleza hayo leo Septemba 20, 2018 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi wakati akiongozwa na wakili Martine Matunda na Ramadhani Maleta kutoa ushahidi wake wa utetezi katika kesi inayomkabili.

Akitoa utetezi wake mahakamani hapo amedai tuhuma anazotuhumiwa nazo zimemuumiza sana kwa sababu alikuwa na ndoto ya kuifikisha TBC mbali ili iweze kutoa gawio kwa Serikali na si Serikali kutoa fedha kwa TBC.

Kuhusu kuisababishia Serikali hasara ya Sh 887.1 milioni, Tido amedai hakushirikishwa kwa namna yoyote katika malipo hayo na kwamba angeshirikishwa angeweza kunusuru pesa hiyo isilipwe.

Amedai mwaka 2012 aliitwa Takukuru kutoa maelezo na kwamba malipo yanaonyesha kufanyika mwaka 2015 yeye akiwa tayari ni mtuhumiwa na hakuwahi kuitwa popote kuulizwa kuhusu mchakato mzima wa mradi kabla malipo hayo hayajafanyika kwani angeweza kushauri.

Tido aliyeanza kujitetea leo Septemba 20 kuanzia saa tatu asubuhi amemaliza utetezi wake saa sita mchana.


from MPEKUZI

Comments