Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Yatuma Salamu za Rambirambi Ajali MV Nyerere

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imetoa salamu za rambirambi kwa ndugu, jamaa na marafiki kwa wananchi wote walioguswa na ajali ya MV Nyerere iliyotokea jijini Mwanza .

Waziri Nchi,  Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Mohamed Aboud Mohamed akitoa taarifa ya Serikali leo Septemba 21,2018 amesema wamepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za ajali ya kivuko hicho iliyosababisha vifo vya baadhi ya wananchi.

Amesema Serikali ya Zanzibar na watu wake wote wanaungana na ndugu wa Tanzania bara katika kipindi hiki kigumu kutokana na ajali hiyo.

"Kwa niaba ya Serikali, tuwatake wale wote walioguswa na ajali hiyo wawe wapole na wastahamilivu katika kipindi hiki kigumu" amesema.

Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Baraza la Wawakilishi, Mwanasha Khamis akitoa taarifa za baraza hilo kwa niaba ya Spika amesema wajumbe wa baraza hilo wamepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za ajali hiyo.

Amesema msiba huo si wa  wana Mwanza pekee bali ni wa Watanzania wote wakiwamo wajumbe wa baraza hilo kwa ujumla.

Amesema kutokana na tukio hilo kubwa ofisi ya Baraza hilo limeahirisha kikao cha jioni ya leo Ijumaa cha Baraza hilo ili kuungana na wenzao katika msiba huo.

"Kwa niaba ya Spika napenda kuchukua nafasi hii kutamka kuwa kikao chetu kilichopangwa kufanyika jioni ya leo, kimehirishwa lengo ni kuungana na wenzetu katika msiba uliotokea" amesema.

Amesema kikao cha Baraza la Wawakilishi kitaendelea tena Jumatatu ya 24 saa tatu za asubuhi.


from MPEKUZI

Comments