Serikali Kuwezesha Vituo Vya Utafiti Ili Kuongeza Uzalishaji Wa Aina Mpya Wa Mbegu Bora

Na Mathias Canal-WK, Arusha
Serikali imeahidi kuendelea kuwezesha vituo vyake vya utafiti kote nchini kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa aina mpya za mbegu bora za mazao mbali mbali.

Kauli hiyo imetolewa na Mhe Dkt Charles Tizeba Waziri wa Kilimo, wakati akifungua mkutano wa siku mbili wa wadau wa mbegu ambapo ni mjumuiko wa Jumuiya ya Wafanyabiashara ya Mbegu (TASTA), TOSCI, USAID East Africa Trade Investment Hub, AGRA-MIRA Project, AATF, ASA na TPRI kwa kushirikiana na wizara ya Kilimo na wadau wengine wa maendeleo unaofanyika katika Ukumbi wa Mount Meru Hotel Jijini Arusha.

Alisema kuwa katika kuhakikisha kuwa Wizara ya kilimo inafikia hatua ya kuwa na uzalishaji Wa aina mpya za mbegu bora za Mazao mbalimbali tayari serikali imechukua hatua ya kuanzisha Taasisi ya Utafiti Wa kilimo - TARI kwa lengo la kuboresha utendaji wa kitafiti ili kuleta tija katika ugunduzi wa aina mpya za mbegu.

Alisema kuwa TARI itasaidia kuongeza uzalishaji wa mbegu bora hapa nchini na hivyo kuwa na matokeo chanya ya uhakika wa chakula katika ngazi ya kaya na Taifa kwa ujumla pia kuongeza kipato kutokana na ziada.

Dkt Tizeba alisema kuwa Mpango wa Kuendeleza sekta ya Kilimo awamu ya pili – ASDP II ambao Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli ameuzindua hivi karibuni unasisitiza masuala ya uendelezaji wa kilimo chenye tija, Kilimo biashara chenye kuboresha mapato ya mkulima na kilimo  kinachomhakikishia mkulima usalama wa chakula na lishe.

"Haiwezi kuwa rahisi kuongeza uzalishaji wa kilimo hapa nchini kama msingi wa kilimo ambao ni uzalishaji wa mbegu bado tutakuwa tumeuacha nyuma pasina kuweka msisitizo hapo, hivyo tunapaswa kutazama upya namna bora ya kupunguza gharama ya mbegu" Alikaririwa Mhe Dkt Tizeba na kuongeza kuwa

"Baada ya serikali kujitoa katika uendeshaji wa biashara mbalimbali na kuruhusu sekta binafsi kufanya biashara, hii ilitoa fursa kwa sekta binafsi kushiriki katika tasnia mbalimbali ikiwemo hii ya mbegu, lengo kuu la dhana hii ya ushirikishaji wa sekta binafsi na ile ya umma (PPP) ni kuwezesha na kuhakikisha kwamba maslahi mapana ya wakulima yanalindwa na mazingira ya biashara yanaboreshwa ili wakulima na sekta binafsi wote wafaidike na jitihada wanazozifanya"

Waziri Tizeba aliongeza kuwa Ili kutekeleza lengo la kuongeza tija na uzalishaji katika sekta ya mbegu, Wizara ya Kilimo kupitia Sheria ya Mbegu ya Mwaka 2003, imeweka mifumo mbalimbali ya namna ya kutoa na kufikisha huduma kwa wakulima kwa kushirikiana na sekta binafsi kwa lengo la kuboresha huduma hizo ili kuongeza kasi ya ukuaji wa maendeleo ya wakulima.

Alizitaja jitihada hizo kuwa ni katika kutekeleza majukumu ya pamoja katika ubia baina ya sekta ya umma na ile ya binafsi. "Lakini kwa bahati mbaya juhudi hizi hazijazaa matunda yaliyotarajiwa na ndiyo maana mpaka sasa bado tunakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo uzalishaji mdogo wa mbegu, uwepo wa mbegu zisizokidhi viwango vya ubora sokoni na kutegemea mbegu za kuagizwa kutoka nje. Hali hii tunatakiwa kuondokana nayo na kuhakikisha tunazalisha mbegu za kutosha mahitaji ya ndani na ziada kuuza nje" Alisistiza Dkt Tizeba

Aidha, alidema juhudi mbalimbali zinaendelea kufanyika kati ya Serikali na Sekta binafsi katika kupambana na uwepo wa mbegu zisizokidhi viwango vya ubora sokoni. Miongoni mwa juhudi hizo ni kuweka karatasi yenye maelezo na utambulisho ‘label’’ katika vifungashio vya mbegu. "Hii ni sehemu ya utekelezaji wa Sheria ya Mbegu ya mwaka 2003 ambapo utekelezaji wake umekuwa na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na malalamiko ya wafanyabiashara kudai kuwa hizo ‘lebel’ zinaongeza gharama. Hivyo napenda kuchukua fursa hii kuwafahamisha wadau wote wa sekta ya mbegu kuwa hilo ni takwa la kisheria hivyo ni budi sote tulizingatie" Alisema

MWISHO.



from MPEKUZI

Comments