Raia Wa Nigeria Kizimbani Kwa Kusafirisha Dawa za Kulevya

Raia wa nchini Nigeria, Martine Ike (46) mfanyabiashara na Mkazi wa Mbezi Salasala, amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na shtaka la kusafirisha gramu 647.7 za dawa za kulevya aina ya Heroin.

Wakili wa Serikali, Faraja Nguka akisoma hati ya mashtaka, leo Septemba 18,2018 mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Augustine Rwizile amedai kuwa mshtakiwa ametenda kosa hilo Julai 6,2018.

Imedaiwa, siku ya tukio, mshtakiwa huyo akiwa katika ofisi ya basi la kampuni ya Tahmeed iliyopo Mwembe Tayari Mombasa nchini Kenya, alikamatwa akisafirisha dawa hizo za kulevya zenye uzito wa gramu 647.7.

Hata hivyo, baada ya mshtakiwa huyo kusomewa shtaka lake, hakuruhusiwa kujibu chochote kwa sababu Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu haina mamlaka ya kuisikiliza kesi hiyo hadi Mahakama Kuu au kwa kupata kibali kutoka kwa DPP.

Kwa mujibu wa upande wa mashtaka upelelezi bado haujakamilika na kesi imeahirishwa hadi Septemba 26 mwaka huu kwa ajili ya kutajwa na kuangalia kama upelelezi utakuwa umekamilika ama la.


from MPEKUZI

Comments