Msako Wa Polisi Jijini Arusha Wafanikisha Kupata Gari Lililoibiwa, Bastola

Na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha
Jeshi la Polisi mkoani hapa limefanikiwa kupata gari lililoibiwa aina ya Toyota Surf lenye namba za usajili T.996 AGK pamoja na Bastola aina ya Browning iliyokuwa na risasi Nane ndani ya Magazine.

Akizungumza na Waandishi wa habari jana mchana  Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Ramadhani Ng’anzi alisema kwamba tukio la kuibiwa kwa gari hilo lililokuwa linaendeshwa na Bi. Sarah Cornel (40) Mwalimu wa Sekondari na ni mkazi wa Olasiti jijini hapa lilitokea Septemba 17 muda wa saa 9:50 Alasiri katika maeneo ya Stand Ndogo.

“Mara baada ya kuegesha gari lake maeneo ya Stendi Ndogo alienda madukani kwa ajili ya kufanya manunuzi aliporudi hakulikuta ndipo alipoelekea kituo Kikuu cha Polisi kwa ajili ya kutoa taarifa ambayo ilifanyiwa kazi kwa kuanza kuweka vizuizi maeneo ya barabara kuu na kufanya msako mkali”.

Alisema wahalifu hao baada ya kuona njia zote zimedhibitiwa waliamua kulitelekeza gari hilo katika kituo cha Afya Kaloleni kilichopo jijini hapa ambapo siku ya pili muda saa 05:30 Asubuhi lilipatikana huku watuhumiwa wakiwa wametoweka na Jeshi hilo linaendelea kufanya uchunguzi wa Kisayansi ili kuweza kuwabaini.

Mbali na tukio hilo Polisi mkoani hapa wameweza kupata silaha aina ya bastola ambayo ilikuwa na risasi nane ndani ya Magazine, Kamanda Ng’anzi alisema lilitokea Septemba 15 mwaka huu katika kijiji cha Kimyaki kilichopo tarafa ya Enaboishu wilayani Arumeru.

Alisema Jeshi hilo lilipata taarifa hiyo toka kwa raia wema ambapo waliwadokeza kuwapo kwa silaha hiyo ndani ya chumba cha mtu waliyekuwa wanamdhania mhalifu ndipo askari walikwenda katika eneo hilo na kufanikikwa kupata silaha hiyo ambayo wanakiri ilikuwa inamilikiwa isivyo halali na Jeshi hilo linaendelea na msako mkali kumtafuta mtuhumiwa huyo.

Mbali na mafanikio hayo msako wa Jeshi hilo umeweza kufanikisha kupata mali mbalimbali zikiwemo TV mbili “flat Screen”, Laptop, Jenereta na vitu vingine ambavyo vinasadikiwa kuibiwa katika mitaa mbalimbali ya jiji la Arusha siku za nyuma.

Kwa upamde wa Usalama barabarani Jeshi hilo limepanga kuanzisha kikosi maalum kwa ajili ya kuwadhibiti waendesha boda boda wanaovunja sheria hasa za kubeba abiria zaidi ya mmoja maarufu kama “Mishikashi” na wale wanaovuka mataa bila kuruhusiwa.

Kamanda Ng’anzi alisema kikosi hicho kitakuwa na askari ambao watakuwa wanavaa kiraia na watasambazwa katika maeneo mbalimbali ya jiji la Arusha hali ambayo anaamini itakomesha tabia ya madereva wa boda boda wanaovunja sheria kwa makusudi.


from MPEKUZI

Comments