Mkurugenzi tume ya Uchaguzi ampa Mbowe siku 7 Aombe Radhi

Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Dr Athumani Kihamia ametoa siku saba kwa Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Freeman Mbowe kumuomba radhi kwa kile alichokidai kiongozi huyo kutoa maneno yaliyoashiria  kumkashifu.

Kwa mujibu Dkt.  Kihamia kwenye mkutano wa Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe na Waandishi wa habari alitamka kuwa mkurugenzi Kihamia akachukue fomu ya kuwania nafasi ya Uongozi katika baadhi ya maeneo ya Uchaguzi kwa madai kiongozi huyo anatumika na Chama Cha Mapinduzi.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam Dkt. Athumani Kihamia amesema Mbowe anatakiwa achague maneno ya kusema.

"Namwambia (Freeman) Mbowe achague maneno ya kuongea yeye ni kiongozi mkubwa wa chama. Achuje maneno yake na awe na ushahidi, mimi sipendi kulumbana na wanasiasa na asitafute kiki,” amesema.

"Mimi sijawahi kukutana naye, lakini nimeshawaambia kina (John) Mnyika na John Mrema wamfikishie ujumbe, mimi si wa kutania," ameongeza.

Dk Kihamia amesema Mbowe asipoomba radhi basi Watanzania wawe makini kutokana na kauli zake.

"Kama alikuwa anatesti mitambo kuwa akitukana hajibiwi, mimi sipo hivyo lazima nitakujibu kwa sababu nipo kwa ajili ya kuhakikisha Nec inajizatiti kutekeleza majukumu yake"

Kuhusiana na hoja zilizolalamikiwa na CHADEMA na kupelekea kujitoa kushiriki kwenye uchaguzi wa marudio utakaofanyika katika jimbo la Liwale na baadhi ya kata Dr  Kihamia amesema; "tume haina mpango wa kuongeza vituo hewa wala kupunguza vituo isipokuwa tunatumia vituo vilevile vya 2015 mpaka tutakapohakiki tena orodha ya daftari la kudumu la wapiga kura."

Jana Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kilitangaza kujiondoa rasmi kushiriki chaguzi ndogo zote zilizotangazwa kufanyika hivi karibuni na chaguzi zozote zitakazofuata zinazosimamiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa madai kwamba tume hiyo inafanya kazi ya Chama Cha Mapinduzi.


from MPEKUZI

Comments