Mgombea CHADEMA Ukonga ahofia kutekwa

Mgombea ubunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) jimbo la Ukonga jijini Dar es salaam Asia Msangi amesema miongoni mwa changamoto anazokutana nazo kuelekea uchaguzi wa marudio jimbo hilo utakaofanyika siku ya jumapili ya  septemba 16, ni hofu ya kutekwa na watu wasiojulikana.

Akizungumza katika kituo cha EATV leo, mgombea huyo wa CHADEMA amesema kupitia viongozi wa juu wa chama chake wamepokea taarifa juu ya uvumi wa kutaka kutekwa siku moja kabla ya zoezi la kupiga kura.

“…Baadhi ya changamoto kwenye uchaguzi huu wa marudio ninazokutana nazo .., kuna baadhi ya watu wetu wanatishiwa kutekwa na kuna mwingine alitekwa ila kwa ushirikiano na mwenyekiti jana amepatikana.., lakini pia kupitia viongozi wa juu wa chama tumepokea taarifa ya mimi kutaka kutekwa kabla ya jumamosi na hili jambo tutalifikisha polisi. ” Amesema Asia Msangi

Aidha Asia Msangi amesema licha ya  miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) kupitia seikali ya awamu ya tano ikiwemo reli ya kisasa (SGR), ununuaji wa ndege pamoja na Shirika la ndege la Tanzania ATCL anaamini miradi hiyo haiwezi kuwa kikwazo cha kutoshinda uchaguzi wa jimbo hilo.

“ Licha ya miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Rais Magufuli bado maisha ya mwananchi mmoja mmoja wa jimbo la ukonga ni magumu.., hiyo miradi haiakisi chochote.., wananchi wa ukonga hawawezi kunufaika..”Ameongeza Asia Msangi

Uchaguzi wa jimbo la Ukonga unarudiwa kufuatia aliyekua Mbunge wa jimbo hilo kupitia CHADEMA Mwita Waitara kutangaza kujivua nafasi hiyo Julai 28 mwaka huu kwa madai ya kuwa na mgogoro na Mwenyekiti wa chama hicho Freeman Mbowe.


from MPEKUZI

Comments