Makonda Awapa Miezi Minne Waajiri Kuhakikisha Wanawaajiri Watu Wenye Ulemavu Kama Sheria Inavyowataka

Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Paul Makonda leo ametoa miezi minne kwa waajiri wa Makampuni na Mashirika kuhakikisha wanawaajiri watu wenye ulemavu Kama Sheria ya Walemavu ya 2010 na Mikataba ya kimataifa ya mwaka 2006 iliyoridhiwa na Tanzania mwaka 2009 sura ya 27 unavyowaaagiza kufanya hivyo.

RC Makonda amesema ifikapo Mwezi January mwakani ataanza ziara ya kutembelea kwenye kila kampuni na taasisi jijini humo kukagua Kama wametekeleza sheria na agizo hilo ambapo watakaobainika kukaidi watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

Aidha RC Makonda amesema kitendo cha kuwaajiri walemavu itapunguza ongezeko la ombaomba,ukatili, utupwaji wa watoto wenye ulemavu, kuhamasisha walemavu kusoma pamoja na kuwawezesha walemavu kuhudumia familia zao.

“Hatuwezi kuwa na ndugu zetu wamesoma na wanasifa za kupata Kazi lakini tunawanyima matokeo yake wengine wanaishia kujinyonga, kinamama wanatupa Watoto wenye ulemavu, mila potovu zinaendelea kupoteza haki na mwisho wanabaki wakiwa Masikini na kushindwa hata kumudu gharama za Matibabu, Jambo hili sio la kufumbia macho” alisema Makonda

Kwa mujibu wa Sheria ya ajira kwa watu wenye ulemavu No. 9 ya mwaka 2010 kifungu cha 31 inamtaka kila mwajiri mwenye wafanyakazi zaidi ya 20 kuhakikisha 3% ya wafanyakazi ni watu wenye ulemavu.


from MPEKUZI

Comments