Jeshi La Polisi Jijini Arusha Lawahakikishia Usalama Wananchi Siku ya Kupiga Kura Kesho

Na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha
Jeshi la Polisi mkoani hapa limesema litaendelea kuimarisha ulinzi katika uchaguzi mdogo wa marudio wa kugombea kiti cha ubunge unaotarajiwa kufanyika kesho Jumapili wilayani Monduli kama jinsi ilivyokuwa kwenye kampeni.

Akitoa taarifa hiyo leo asubuhi, Kamanda wa Polisi mkoani hapa Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Ramadhani Ng’anzi, alisema wananchi wenye sifa za kupiga kura wajitokeze kwa wingi katika vituo vya kupigia kura kwani Jeshi hilo limezidi kuimarisha ulinzi ili uchaguzi huo ufanyike kwa amani na utulivu.

“Kama ilivyo kwenye kampeni hali ilikuwa tulivu na wakati wa uchaguzi tutahakikisha kwamba hali hii inaendelea kuwa shwari, askari toka vikosi mbalimbali watakuwepo wilayani hapo kwa ajili ya kuhakikisha uchaguzi unafanyika katika hali ya usalama.” Alilisitiza Kamanda Ng’anzi.

Aidha aliwataka wananchi wa jimbo la Monduli mara baada ya kutimiza haki yao msingi ya kupiga kura wasikae kwenye vituo kwani hali hiyo inaweza kusababisha vurugu.

Kamanda Ng’anzi aliwaonya baadhi ya watu wanaopanga kufanya fujo wakati wa uchaguzi au mara baada ya uchaguzi kumalizika watakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria na kusisitiza kuwa yeye mwenyewe atakuwepo wilayani humo kwa ajili ya kujionea na kusimamia kwa karibu shughuli za Usalama katika kipindi chote cha kupiga kura hadi kutangaza matokeo.

“Ole wao watakaopanga kufanya vurugu, Jeshi la Polisi lipo imara na halitashindwa kumkamata yeyote atakayeshawishi au kufanya fujo katika uchaguzi huo ambao tunategemea utakuwa wa amani na utulivu”. Alimalizia kwa kuonya Kamanda Ng’anzi.


from MPEKUZI

Comments