Jela Miaka 6 Kwa Kumkashifu Rais Magufuli

Yuston Emanuel (31) mkazi wa Ngara mkoani Kagera amehukumiwa kwenda jela miezi sita au kulipa faini ya Sh200, 000 kwa kosa la kutumia lugha ya dhihaka dhidi ya Rais John Magufuli.

Hukumu hiyo ilitolewa leo na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi  Septemba 17, 2018 wilaya ya Misungwi, Erick Marley baada ya kuridhika bila shaka yoyote na ushahidi wa upande wa Jamhuri kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo.

Katika shauri hilo la jinai namba 27/2018, upande wa Jamhuri ulioongozwa na mwendesha mashitaka wa polisi, Ramsoney Salehe uliita mashahidi watano kuthibitisha kosa.

Akisoma maelezo ya kosa, mwendesha mashitaka huyo aliiambia Mahakama mshtakiwa alitenda kosa hilo saa 10:00 jioni ya Juni 25 akiwa eneo la kivuko cha Kigongo wilayani Misungwi.

Alidai akiwa eneo hilo, mshtakiwa aliyekuwa akivuka kutoka Kigongo wilayani Misungwi kwenda Busisi wilayani Sengerema alitumia maneno ya dhihaka dhidi ya Rais John Magufuli kwa kutamka "Rais Magufuli kitu gani bwana"

Salehe aliiambia mahakama kosa hilo ni kinyume cha kifungu cha 89 (1) (a) kanuni ya adhabu iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

“Naiomba Mahakama itoe adhabu kali ili iwe fundisho kwa wengine wanaotoa lugha ya kumdhihaki Rais Magufuli kama alivyofanya mshtakiwa ambaye Rais (Rais John Magufuli) anaweza kuwa mzazi wake,” alisema Salehe.

 Akijitetea baada ya kutiwa hatiani, mshtakiwa aliiomba Mahakama kumpunguzia adhabu na kumsamehe kwa sababu ni kosa lake la kwanza.

Mpaka muda wa Mahakama unamalizika jana, mshtakiwa alishindwa kulipa faini na hivyo kupelekwa gereza kuanza kutumikia kifungo cha miezi sita jela.


from MPEKUZI

Comments