James Mbatia: Tunayo Yashuhudia Ajali ya MV Nyerere ni Aibu Tupu....Unawezaje Kusitisha Uokoaji Kisa Giza?

Ajali ya kivuko cha MV-Nyerere iliyotokea wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza na kusababisha  vifo  vya mamia watanzania waliokua wakisafiri kupitia kivuko hicho imemuibua Mwenyekiti wa Chama Cha NCCR-Mageuzi na Mbunge wa jimbo la Vunjo James Mbatia

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam Mbunge wa huyo ameikosoa kauli ya mkuu wa mkoa wa Mwanza Joel Mongela kuwa zoezi la Uokoaji lilisimamishwa kwa sababu ya giza.

“Hii ni ajali ya kujitakia, haingii akilini kwa  historia ya majanga nchini, ni aibu kuona shughuli za uokoaji zinasimamishwa kwa sababu ya giza, inatia uchungu inaumiza, Tanzania ni yetu sote.

“Ukiacha ajali hii ya kivuko, meli za MV Spice Islanders na MV Bukoba ambazo zote zilizama, zilikuwa elimu tosha na hizi ajali za meli kuzama hazikupaswa kutokea tena.

“Ukikusanya ajali hizi ukiwa na takwimu sahihi za kutosha na rejea ya majanga unaweza kujua jinsi ya kuokoa raia, kulinda raia ili yasitokee tena majanga badala ya kulalamika na  kunyoosheana vidole,  kushikana mashati.” Amesema Mbatia

Amesema ajali za aina hiyo zinapotokea, wengi huishia kutoa pole jambo ambalo halisaidii.

Mbatia ameshauri kuanzishwa kwa sheria ya wakala wa usimamizi wa maafa kwa lengo la kuwalinda na kuwakinga wananchi.

"Kupanga ni kuchagua, kama walikuwepo wa Chadema walikufa, wa CUF walikufa wa NCCR walikufa, kitengo hicho licha ya kupigiwa kelele hakikuundwa na wanaozungumza ni Polisi, Mkuu wa Mkoa siyo watu maalumu wa maafa wenye elimu ya masuala hayo,” amesema.

"Mara nyingi ninazungumza  bungeni kuikumbusha Serikali wajibu wake namba moja wa kulinda raia. Siasa na kubezana kunapoteza maana.”

Mbatia alimtolea mfano mbunge wa Ukerewe (Chadema), Joseph Mkundi aliyeonya juu ya kivuko hicho kuwa hakikuwa katika hali nzuri, hakuna aliyejali mpaka imetokea ajali hiyo.


from MPEKUZI

Comments