CHADEMA Kuwashitaki Mawaziri Waliopiga Kampeni Monduli

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHEDEMA) kanda ya Kaskazini, kimelalamikia kitendo cha mawaziri kujitokeza na kufanya kampeni za uchaguzi mdogo jimbo la Monduli na kimeeleza kitawafikisha kwenye kamati ya maadili ya taifa.

Katibu wa chama hicho kanda ya Kaskazini ambaye pia ni mwenyekiti wa chama mkoa wa Arusha, Amani Golugwa amesema mbali na malalamiko yao ya kutotendewa haki katika uchaguzi uliofanyika jana lakini watawashtaki mawaziri waliopiga kampeni.

''Sisi kama viongozi tulijipanga vyema kuanzia kampeni tumeona uvunjivu wa sheria mwingi na tumerekodi kila kitu ikiwemo mawaziri kuja kufanya kampeni huku wakiahidi utekelezaji wa miradi kitu ambacho ni kinyume na sheria ya uchaguzi hivyo tutawafikisha kwenye kamati ya taifa ya maadili'', amesema.

Amani Golugwa amewataja baadhi ya mawaziri waliofika jimboni Monduli wakati wa kampeni na kutoa ahadi ni pamoja na waziri wa Ardhi William Lukuvi, Naibu Waziri wa Maji Jumaa Aweso, pamoja na Naibu waziri wa Madini Mhe. Doto Mashaka Biteko.

Aidha Golugwa amefafanua kuwa katika kipindi hicho cha kampeni walishuhudia mawaziri hao wakitoa ahadi na kufanya baadhi ya mambo ambayo kimsingi yapo kinyume na sheria na taratibu za uchaguzi.


from MPEKUZI

Comments