Benki Kuu ya Tanzania (BOT) Yasema ni kosa la jinai kudhihaki au kukejeli noti na sarafu za Tanzania.

Benki Kuu ya Tanzania imewataka wananchi kuheshimu fedha ya Tanzania kwani ni moja ya alama ya taifa.

Kauli hiyo imekuja kufuatia matukio ya hivi karibuni ya baadhi ya wananchi kutoziheshimu, kuzifanyia dhihaka na kebehi noti za Jamhuri ya Mungano wa Tanzania.
 
Taarifa ya BoT kwa vyombo vya habarI ambayo inasema utunzaji mzuri wa fedha zetu utapunguza uwezekano wa fedha hizo kuchakaa mapema na kupunguza gharama za uchapishaji.

"Kwa mujibu wa Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania ya mwaka 2006, kifungu cha 26, BoT ndiyo taasisi pekee yenye mamlaka ya kutoa noti na sarafu katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania," imesema taarifa hiyo.

Pia imesema noti na sarafu hizo zina alama muhimu inayolitambulisha taifa la Tanzania ambayo ni nembo ya Bwana na Bibi. Imefafanua alama hiyo inapaswa kuheshimwa kama zilivyo alama nyingine kwa mfano Bendera ya Taifa.

Pia noti na sarafu zote zimetengenezwa kutoa thamani ya kisheria (legal tender) kama ilivyoandikwa juu ya noti au sarafu husika na pia Benki Kuu pekee ndiyo yenye mamlaka ya kuharibu noti na sarafu.

Taarifa hiyo imefafanua kuhusu hilo kupitia kifungu cha  28 kikisomwa pamoja na kifungu cha 30 cha Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania ya mwaka 2006.

"Benki Kuu inatoa rai kwa wananchi kuzitunza fedha zetu kwa kuwa ni mojawapo ya tunu na alama muhimu ya uchumi wa nchi yetu.

"Vilevile, utunzaji mzuri wa fedha zetu utapunguza uwezekano wa fedha hizo kuchakaa mapema na kupunguza gharama za uchapishaji," imesema taarifa hiyo ya BoT.

==>>Hapo chini ni taarifa ya BoT


from MPEKUZI

Comments