Ajinyonga Baada ya Kuwaua Kwa Mapanga Watoto Wake Wawili

Mkazi wa Chanika jijini Dar es salaam, Dotusi Isaya anadaiwa kuwaua watoto wake wawili, kumjeruhi kwa panga mkewe pamoja na mama mkwe, kisha kujiua baada ya kukataliwa kuwachukua wanae.

Akizungumzia tukio hilo, kamanda wa polisi Mkoa wa Lindi, Pudensiana Protas amesema Isaya alifanya mauaji hayo usiku wa kuamkia jana huko Nachingwea mkoani humo ambapo mtuhumiwa alikwenda Nachingwea anakoishi mkewe Mariam Lucas na kujificha pembeni mwa nyumba ambayo haijamaliza kujengwa (pagala) akimvizia kisha kumkata panga eneo la kisogo na begani.

“Baada ya kumkata mkewe aliingia ndani ya nyumba (katika) chumba wanacholala watoto na kukuta wanawe wawili wamelala na watoto wengine, lakini yeye aliwaua wanawe kwa kuwakatakata”, amesema Kamanda.

Kamanda amesema kuwa Isaya ameamua kufanya tukio hilo baada ya mkewe kumkatalia asiende na watoto wake Bukoba baada ya kuondoka jijini Dar es salaam walikokuwa wakiishi awali, ambapo mke wake alimwambia mume wake kuwa watoto wakiwa wakubwa atawachukua, lakini kwa sasa ataendelea kuishi nao kwa kuwa bado ni wadogo.

Kamanda ameongeza kuwa kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, wamesema walianza kusikia vilio saa sita usiku na walipofika eneo la tukio waliwakuta majeruhi wawili (Amanda na Mariam) pamoja na maiti za watoto wawili pamoja na mtuhumiwa akiwa amejinyonga.

Hilo si tukio la kwanza la mzazi kuua watoto wake kwani Aprili 2017, mkazi wa Bukoba, Respicius Deogratius aliwaua wanaye mapacha waitwao Nyakato na Nyangoma kwa kuwakata vichwa.

Tukio jingine ni la Aprili mwaka huu ambapo Pius Salum, mkazi wa Matai, Kalambo mkoani Rukwa alimuua mtoto wake, Benedicto Salum (13) kwa kumpiga ngumi na mateke tumboni akidai si wake.


from MPEKUZI

Comments