Ahukumiwa Miaka 30 Jela Kwa Kumbaka Mtoto Bubu

Mahakama  ya Wilaya ya Mpanda mkoani Katavi, imemhukumu Ramadhani Shaban (24), Mkazi wa Mtaa wa Majengo B, kifungo cha miaka 30 jela, baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kumbaka mtoto mwenye umri wa miaka 15, bubu ambaye pia ana upungufu wa akili.

Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Gosper Luoga, baada ya mshtakiwa kukiri kosa.

Awali, Mwendesha Mashtaka wa Serikali wa Mkoa wa Katavi, Flaviana Shio, alidai mahakamani hapo kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo Septemba 9, mwaka huu majira ya saa 12 jioni katika Mtaa wa Majengo B.

Alidai kuwa siku ya tukio mshtakiwa alikwenda maeneo ya Mtaa wa Mjimwema alikokuwa akiishi mtoto huyo na mjomba wake, Ernest Chambala na kumpakia kwenye baiskeli yake.

Alisema alikwenda naye hadi kwenye chumba chake alichokuwa amepanga na kumbaka.

Aliendelea kuiambia mahakama kuwa baada ya tukio hilo mtoto huyo alitoka nje na kuanza kuwaonyesha watu kwa ishara kuwa amebakwa.

Mjomba wa mtoto huyo alianza jitihada za kumsaka mbakaji huyo kwa kumchukua mpwa wake huyo ambaye alimwongoza hadi kwenye nyumba alikofanyiwa unyama huo.

Alieleza kuwa majirani wa nyumba hiyo walipoulizwa kama walimuona mtoto huyo akiingizwa kwenye chumba cha mshtakiwa walikiri kumuona.

Baada ya kukamatwa alichukuliwa na kupelekwa kituo cha polisi na katika maelezo yake alikiri kutenda kosa hilo na taarifa za daktari zilithibitisha kuwa mtoto huyo alikuwa ameingiliwa na mwanaume kwa kuwa sehemu zake za siri zilikuwa na mbegu za kiume.

Mshtakiwa alikiri kutenda kosa hilo kwa kile alichodai amekuwa akifanya naye mapenzi mara kwa mara kwa sababu ni mpenzi wake.

Katika utetezi wake, mshtakiwa aliiomba mahakama impunguzie adhabu kwa kuwa mama yake mzazi anamtegemea na baba yake alishafariki.

Hakimu Luoga baada ya kusikiliza utetezi huo aliiambia mahakama kuwa mshtakiwa amepatikana na hatia imemhukumu kwenda kutumikia jela miaka 30.

Alisema katika hukumu hiyo mahakama pia imezingatia ongezeko la matukio ya ubakaji wilayani humo.



from MPEKUZI

Comments