Agizo la Rais Magufuli Laanza Kutekelezwa....Nemc, Mkemia Mkuu wa Serikali wachukua sampuli maji yenye Sumu

Wataalamu  kutoka Baraza la Usimamizi wa Mazingira nchini (NEMC) kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, wamechukua sampuli zaidi ya kumi ya maji kutoka katika vyanzo mbalimbali kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi, ili kuona kama maji hayo yana kemikali zenye madhara kwa viumbe hai.

Sampuli ya maji hayo yanayodhaniwa kuwa na kemikali yanayotiririka kutoka katika mgodi wa Acacia North Mara mpaka kwenye makazi ya watu.

Uchukuaji wa sampuli hizo ni utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli alilolitoa hivi karibuni alipokuwa ziarani mkoani Mara.

Akizungumza wakati zoezi hilo likiendelea, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dk. Vedast Makota, alisema kuwa NEMC imeanza kutekeleza agizo hilo kwa kuchukua sampuli katika maeneo yote ili kubaini kama zina madhara kwa viumbe hai au la.

“ NEMC kwa kushirikiana na ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali watafika kila mahala ikiwamo kupitia vibali vyote vya awali ili kubaini kama utolewaji wa vibali hivyo ulikidhi vigezo vinavyotakiwa na kuona kama wamiliki wa mgodi huo wanazingatia masharti yaliyoagizwa katika vibali hivyo,” Dk. Makota alisisitiza.

Alisema utafiti wao utaenda sambamba na uchukuaji sampuli mbalimbali yakiwamo maji, mimea na mchanga ambapo watahakikisha wanashirikiana na jamii inayozunguka mgodi huo ili kufanikisha zoezi zima kuona kama kuna viashiria vinavyoshukiwa kuwa na chembe chembe zenye kemikali.

“Tupo katika hatua za awali za utekelezaji wa agizo hilo ambapo wataalamu wametembelea maeneo ya Mto Tigite, ambao kwa kiasi kikubwa maji yake ndiyo yanatumika sana kwa wakazi wa eneo hilo katika shughuli mbalimbali za kijamii,” alisema.

Alisema wameshatembelea mabwawa mbalimbali yanayotumika kuhifadhia tope sumu (TFS) zinazotokana na shughuli za mgodi huo, ikiwamo wataalamu kutoka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kuchukua sampuli mbalimbali ambazo zitapelekwa maabara kwa ajili ya kufanyiwa vipimo vya kitaalamu.

“Baada ya kukamilisha zoezi la utafiti na uchukuaji sampuli hizo na kubaini ukiukwaji wa sheria za mazingira ni wazi kuwa NEMC haitosita kuchukua hatua kali za kisheria kwa mmiliki ili iwe fundisho kwa wengine,” alisema.

Naye Meneja wa Kanda Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Venkya Masambu, alisema kwa kutambua uharibifu mkubwa unajitokeza katika maeneo ya migodini, ofisi yake kwa kushirikiana na NEMC waliamua kuchukua sampuli hizo upya ambazo watazipeleka katika maabara ya serikali yenye wataalamu waliobobea.

“Endapo sampuli zitakazopelekwa kwa Mkemia Mkuu zitabainika kuwa na madhara kwa binadamu hawatasita kutoa ushauri kwa wamiliki wa mgodi, ili kuona namna gani ya kutatua dosari zinazoweza kujitokeza,” alisema.

Mratibu wa Uendeshaji Idara ya Uchenjuaji Dhahabu wa Acacia North Mara, Patice Kabazimu, alisema wamewapokea wataalamu hao na watahakikisha wanawapatia ushirikiano wa kutosha kufanikisha kazi yao.

“Sisi kama Acacia tunatambua umuhimu wa zoezi linalofanywa na wataalamu hawa ili kuleta ustawi na maendeleo kwa jamii yetu,” alisema.


from MPEKUZI

Comments