Waziri Mkuu Kuanza Ziara Ya Siku 3 Mkoani Tabora Kesho

Na Tiganya Vincent
Waziri Mkuu  Kassim Majaliwa anatarajia kuanza ziara ya kikazi ya siku tatu mkoani Tabora ambapo atawasili mkoani  humo kesho.

Baada ya Waziri Mkuu kuwasili atapokelewa na viongozi wa Serikali na kusomewa taarifa ya Mkoa wa Tabora.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri Waziri Mkuu atatembelea Wilaya ya Igunga, Nzega na Manispaa ya Tabora kwa ajili ya kuzungumza na wananchi, watumishi wa umma na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo.

Alisema kuwa akiwa wilayani Igunga atazungumza  na wakazi wa Jimbo la Igunga , Manonga na watumishi wa umma na kukagua Kiwanga cha Pamba cha Manonga.

Mwanri aliongeza kuwa baada ya kutoka Igunga Waziri Mkuu atakwenda Nzega na kuzungumza na wananchi wa Jimbo la Bukene, Nzega Mjini na Nzega na watumishi wa umma.

Alisema Waziri Mkuu atakamilisha ziara yake katika Manispaa ya Tabora kwa kuzungumza na Watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Manispaa ya Tabora na Hospitali ya Rufaa Kitete na kukagua maendeleo ya Chuo cha Afya katika Hospitali ya Rufaa Kitete.

Mwanri alisema Waziri Mkuu pia atapata fursa ya kutembelea Kiwanda cha Nyuzi (Tabora Textile) , Kiwanda cha Maziwa na kuongea na wananchi wa Jimbo la Tabora kabla ya kuondoka na kuendelea na majukumu mengine ya ujenzi wa Taifa.

Alitoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kumlaki Waziri Mkuu na kumsikiliza na kuwa tayari kupokea maagizo atakayotoa.


from MPEKUZI

Comments