TRA Yatoa Elimu Ya Kodi Kwa Washiriki Wa Jukwaa La Fursa Za Biashara Geita

Na Veronica Kazimoto
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imewaelimisha wafanyabiashara na wadau mbalimbali walioshiriki Jukwaa la Fursa za Biashara mkoani Geita na kuwafafanulia juu ya masuala mbalimbali yanayohusu kodi ikiwa ni pamoja na msamaha wa riba na adhabu kwenye malimbikizo ya madeni ya kodi. 
 
Akizungumza wakati akiwasilisha mada kuhusu kodi katika jukwaa hilo, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa mamlaka hiyo amewataka wafanyabiashara wenye malimbikizo ya madeni ya kodi na wale wote waliokuwa wakifanya biashara bila kusajiliwa  kuchangamkia msamaha huo ipasavyo kwani hilo ni zoezi la miezi sita pekee.

"Nachukua fursa hii kutoa wito kwa wafanyabiashara wote wenye malimbikizo ya madeni ya kodi na wote waliokuwa wakifanya biashara bila kusajiliwa kuwasilisha maombi yao TRA ili waweze kupata msamaha huu wa riba na adhabu wa asilimia 100 ambapo mwisho wa kutuma maombi ni tarehe 30 Novemba, 2018.

Aidha, Mkurugenzi Kayombo amewahimiza wafanyabiashara wadogo waliopo kwenye utaratibu wa makadirio kusajiliwa na kupatiwa Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) ambayo hutolewa na TRA bure bila ulazima wa kulipa kodi ya awamu ya kwanza kabla ya kuanza biashara isipokuwa ndani ya siku 90 baada ya kuanza biashara.

 “Awali wafanyabiashara walikuwa wanalipa kodi mara tu baada kusajili biashara zao na kukadiriwa kodi, lakini sasa hivi tumeweka utaratibu wa kulipa kodi ndani ya siku 90 kwa awamu ya kwanza baada ya kusajiliwa na na kuanza biashara, alifafanua Kayombo.

Pamoja na mambo mengine, Kayombo amewakumbusha wafanyabiashara na washiriki wa jukwaa hilo la fursa za biashara suala zima la kutoa risiti za kielektroniki za EFD kila wanapouza bidhaa na huduma mbalimbali na kudai risti kila wanafanya manunuzi.

Vilevile, amewasisitiza wafanyabiashara wote wa Mkoa wa Geita na wilaya zake wenye changamoto mbalimbali wasisite kuonana na Meneja wa TRA mkoani humo kwa ajili ya kupata ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili ili waweze kufanya biashara zao kwa uhuru.

Jukwaa la Fursa za Biashara limeandaliwa na Ofisi ya Mkoa wa Geita kwa kushirikiana na Shirika la Magazeti ya Serikali (TSN) ambapo Mamlaka ya Mapato Tanzania imeshiriki jukwaa hilo kwa ajili ya kutoa elimu ya kodi kwa wafanyabiashara na wadau mbalimbali hususani wa mkoani hapa.



from MPEKUZI

Comments