RC Songwe Brigedia Jenerali Mwangela Akataa Ombi La Mkandarasi Kuongezewa Muda

Na Grace Gwamagobe -Afisa Habari Songwe
Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brigedia Jenerali Nicodemas E Mwangela amekataa ombi la Mkandarasi kutoka kampuni ya Mats Engineering Ltd Paulo Philipo Paulo la kuongezewa kipindi cha miezi miwili ili aweze kukamilisha ujezi wa Daraja la Kikamba Wilayani Songwe.

Brigedia Jenerali Mwangela amekataa ombi hilo jana alipokagua ujenzi wa daraja la Kikamba linalounganisha kata za Kapalala na Gua wilayani Songwe kwakuwa sababu alizotoa mkandarasi huyo hazijitosheleji.

Alisema daraja hilo lazima likamilike kwa muda uliopangwa ambao ni Septemba, 2018 huku mkandarasi huyo akitoa sababu kuwa atachelewa kukamilisha ujenzi huo kutokana na mvua nyingi zilizonyesha na mwamba mgumu uliopo eneo la ujenzi.

“Mkandarasi ahakikishe anafanya kazi mchana na usiku ili akamilishe ndani ya muda wa mkataba, vifaa vya kumuwezesha kufanya hivyo anavyo na ombi la kuongezewa muda wa ujenzi mimi siafikiani nalo”, alisema Brigedia Jenerali Mwangela.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Songwe Samuel Jeremia alisema yeye na viongozi wengine wataendelea kusimamia miradi ya maendeleo na katika ujenzi wa daraja hilo watahakikisha wanamsimamia mkandarasi huyo ili amalize ndani ya muda uliopangwa.

Daraja la Kikamba linalolunganisha kata za Kapalala na Gua limeanza kujengwa mwezi Oktoba 2017 na linatarajiwa kukamilia Septemba 2018 likiwa limegharimu shilingi bilioni 1.4.



from MPEKUZI

Comments