Profesa Kabudi Atema Cheche Dodoma......Akerwa na maamuzi kufanyika bila Ofisi ya Mwanasheria Mkuu kuarifiwa

WAZIRI wa Katiba na Sheria, Prof. Palamagamba Kabudi amesema kuanzia sasa mawakili walioko kwenye Ofisi ya Mwanasheria Mkuu na wanasheria wote katika Wizara, Mamlaka za Serikali za Mitaa na taasisi za Serikali watakuwa ni Mawakili wa Serikali.

Ametoa kauli hiyo jana mchana (Jumatano, Agosti 15, 2018) kabla hajamkaribisha Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ahutubie wageni waliohudhuria uzinduzi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali jijini Dodoma.

“Kwa miaka mingi kumekuwa na ombwe la usimamizi wa wanasheria walio kwenye utumishi wa umma. Maamuzi mengi yamekuwa yakifanyika pasipo Ofisi ya Mwanasheria Mkuu kuwa na taarifa. Mambo yanapoharibika ndio Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inataarifiwa ili kuokoa jahazi,” alisema.

Alisema hali hiyo kwa miaka mingi imekuwa ikiisababishia Serikali kuingia kwenye migogoro na kuingia hasara. “Baada ya mabadiliko haya, wanasheria wote walioajiriwa katika utumishi wa umma wanakuwa wanafanya kazi na kutumia mamlaka ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ndani ya wizara zao, taasisi zinazojitegemea na Mamlaka za Serikali za Mitaa,” alisema.

“Vilevile wanasheria hao watakuwa chini ya uangalizi wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Nia ya mabadiliko haya ni kumuwezesha Mwanasheria Mkuu wa Serikali awe na usimamizi juu yao na kuwazuia kufanya kazi bila kufuata maelekezo ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.”

Prof. Kabudi alisema mashirika yote ya kimkakati kama vile Bandari, TANESCO nayo pia yataletwa chini ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili kuepuka kuitia Serikali hasara. “Serikali imewekeza fedha nyingi kwenye mashirika haya, lakini kuna maamuzi yanafanyika wakati Ofisi ya Mwanasheria Mkuu haina taarifa,” amesema.

“Kutokana na  marekebisho hayo, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali itaratibu na kusimamia Mawakili wa Serikali walio katika Ofisi hiyo na wanasheria wote katika Wizara, mamlaka za serikali za mitaa na taasisi za Serikali ambao sasa watakuwa ni Mawakili wa Serikali. Aidha, Mawakili wa Serikali walio katika Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali watakuwa chini ya uratibu na usimamizi wa Mkurugenzi wa Mashtaka na Wakili Mkuu wa Serikali,” amesema.

Amesema marekebisho hayo yanatokana na marekebisho ya muundo wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kupitia matangazo ya Serikali Na. 48, 49 na 50 ya tarehe 13 Februari, 2018.

“Leo tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kufanya marekebisho hayo. Rais alianzisha Ofisi huru ya Taifa ya Mashtaka kuchukua nafasi ya iliyokuwa Divisheni ya Mashtaka chini ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Vilevile, Rais alianzisha Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kwa ajili ya kutekeleza majukumu ya usimamizi na uendeshaji wa mashauri ya madai yakiwemo ya kikatiba ambayo Serikali ni mdaawa ambayo awali yalikuwa yakishughulikiwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali,” amesema.

Amesema marekebisho hayo yanakusudia kuongeza ufanisi katika uendeshaji wa mashtaka ya jinai nchini hususani utekelezaji wa azma ya Serikali ya kutenganisha shughuli za upelelezi na uendeshaji wa mashtaka. “Kuanzishwa kwa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kunalenga kuimarisha usimamizi na uendeshaji wa mashauri ya madai na pia kuiwezesha Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuimarika katika weledi na ubobezi wa kitaalamu katika kuishauri Serikali na kuandika Miswada ya Sheria kwa kuzingatia mabadiliko makubwa katika tasnia ya sheria kitaifa, kikanda na kimataifa,” ameongeza.

Hata hivyo, Prof. Kabudi alionya kwamba mabadiliko yoyote hayawezi kuleta matokeo yaliyokusudiwa kama watendaji hawatabadili mtizamo wao. Ni kweli muundo uliobadilishwa ulikaa kwa miaka mingi na inawezekana mambo mengi yalikuwa yanafanyika kwa mazoea. “Kutokana na mabadiliko haya, tunakiri kuwa mitizamo yetu na ya watumishi wenzetu lazima ibadilike. Tumejipanga kuhakikisha kuwa watumishi hawafanyi kazi kwa mazoea ili wasiwe na tashwishwi wala ajizi katika kutekeleza majukumu ya umma.”

“In public service, learn to swallow your pride. In public service, learn to learn your limits. In public service, learn to obey the authority above you, and if you don’t, resign and quit,” alisisitiza.

“Tumejipanga kufanya kazi kwa weledi na katika hili tutaweka mikakati ya kuwaongezea watumishi wa ofisi hizi ujuzi katika maeneo mahususi, na katika hilo tutaweka mipango ya kuwafanyia placement ndani na nje ya nchi ili wapate ujuzi mahususi na kuhakikisha wanapata mafunzo ya muda mfupi na mrefu katika maeneo mbalimbali.

Alisema wameanza mkakati wa kuanzisha umoja wa wanasheria walio katika utumishi wa umma ili kuwawezesha kukutana mara kwa mara na kwamba Agosti 30-31 mwaka huu, wanatarajia kufanya mkutano huo ili kuwaunganisha wanasheria wote wajione wanafanya kazi moja na katika Serikali moja.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU


from MPEKUZI

Comments